Guelleh (73) ashinda muhula wa 5 wa uchaguzi wa rais Djibouti
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i68868-guelleh_(73)_ashinda_muhula_wa_5_wa_uchaguzi_wa_rais_djibouti
Rais Ismail Omar Guelleh wa Djibouti ameibuka mshindi katika uchaguzi mkuu uliofanyika jana Ijumaa.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Apr 10, 2021 03:13 UTC
  • Guelleh (73) ashinda muhula wa 5 wa uchaguzi wa rais Djibouti

Rais Ismail Omar Guelleh wa Djibouti ameibuka mshindi katika uchaguzi mkuu uliofanyika jana Ijumaa.

Hayo ni kwa mujibu wa matokeo ya muda yaliyotangazwa mapema leo Jumamosi na Waziri wa Mambo ya Ndani ya nchi hiyo, Moumin Ahmed Cheick. 

Waziri huyo ameliambia taifa kupitia kanali ya televisheni ya dola RTD kuwa, Rais Guelleh amepata kura 167,535 ambayo ni sawa na asilimia 98 ya kura zilizopigwa katika uchaguzi wa jana uliosusiwa na chama kikuu cha upinzani.

Rais Guelleh amechuana na limbukeni wa kisiasa, Zakaria Ismail Farah (56) ambaye ameambulia kura 5,000, baada ya vyama vikuu vya upinzani nchini humo kususia uchaguzi huo. 

Waangalizi huru wa uchaguzi wamesema zoezi hilo limefanyika vizuri pasi na kuripotiwa kesi yoyote ya udanganyifu au uchakachuaji wa matokeo. Matokeo hayo yanatazamiwa kuthibitishwa na Baraza la Katiba la nchi hiyo.

Ramani inayoonesha nchi ndogo ya Djibouti iliyopakana na Eritrea

Rais Guelleh mwenye umri wa miaka 73 na ambaye amekuwa madarakani tokea mwaka 1999, alishinda tena kiti hicho kwa asilimia 86 katika uchaguzi wa mwaka 2016.

Djibouti ambayo ni nchi ndogo ya Pembe ya Afrika yenye idadi ya watu wasiofikia hata milioni moja, mwaka 2011 ilishuhudia wimbi la maandamano ya kupinga kuchaguliwa tena Rais Guelleh ambaye ilisemakana kuwa alipata asilimia 80 ya kura zilizopigwa. Maandamano hayo yalijiri baada ya Rais Guelleh kuifanyia marekebisho katiba ya nchi, ili kumruhusu kugombea kiti hicho kwa mara ya tatu mfululizo.