Takwa na sisitizo la kuondoka vikosi vya kigeni nchini Libya
Baada ya kupita miezi kadhaa tangu kuanza mwenendo wa amani nchini Libya na kuweko juhudi kubwa za kuitisha uchaguzi wa nchi hiyo baadaye mwaka huu, uwepo wa vikosi vya kigeni na vituo vyao vya kijeshi kumeendelea kuwa kikwazo katika njia hiyo.
Kuhusiana na hilo, Najla al-Manqoush, Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Libya ametoa mwito kwa vikosi vya kijeshi vya nchi za kigeni pamoja na wapiganaji mamluki kuondoka katika ardhi ya nchi hiyo ya kaskazini mwa Afrika wakati inajiandaa na uchaguzi baadaye mwaka huu. Mchakato wa amani nchini Libya ulianza katika miezi ya hivi karibuni kwa usimamizi wa Umoja wa Mataifa ukishirikiana na baadhi ya mataifa na hatimaye ukazaa matunda baada ya kuundwa na kuanza kazi serikali ya mpito ya nchi hiyo.
Miongoni mwa majukumu ya serikali hiyo ni kurejesha usalama na amani, kuileta pamoja mirengo ya kisiasa ya nchi hiyo na kuandaa na kusimamia uchaguzi. Kwa mujibu wa makubaliano yaliyofikiwa, uchaguzi mkuu wa Libya umepangwa kufanyika tarehe 24 Disemba mwaka huu. Ili kufikia hilo, serikali ya mpito ya Libya imeandaa mikakati maalum. Hata hivyo moja ya matatizo makubwa kwa sasa kwa ajili ya kufikia malengo yake ni uwepo wa vikosi vya kigeni pamoja na kambi za kijeshi za madola ajinabi katika nchi hiyo ya kaskazini mwa Afrika.
Kutokuweko serikali kuu yenye nguvu, kukosekana uthabiti wa kisiasa na kiuchumi sambamba na kuibuka vita vya ndani kwa upande mmoja na kuweko kivutio kikubwa nchini Libya kutokana na nchi hiyo kuwa na utajiri mkubwa wa mafuta sambamba na nafasi yake ya kistratejia iliyonayo kwa upande wa pili, ni mambo ambayo yanatajwa na weledi wa mambo kwamba, yamechangia kuweko uingiliaji wa kigeni katika masuala yake ya ndani huku kila dola miongoni mwa madola hayo ya kigeni likitaka hisa yake katika nchi hiyo kwa siri na kwa dhahiri. Mintarafu hiyo, hali hiyo imeigeuza Libya na kuwa medani ya vita vya niaba vya mataifa mbalimbali.
Takwimu za karibuni kabisa zinaonyesha kuwa, nchini Libya kuna wapiganaji zaidi ya 20,000 wa kigeni pamoja na mamluki ambapo akthari ya wapiganaji hao wameingia nchini humo wakitokea Syria na wamekuwa wakiungwa mkono na serikali ya Uturuki. Adha nchini Libya kuna vikosi pia kutoka Imarati.
Najla al-Manqoush, Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa ya Libya sambamba na kusisitiza kwamba, vikosi vyote vya kigeni vinapaswa kuondoka katika nchi hiyo amesema kuwa: Sisi tuna azma thabiti katika malengo yetu na tunataka mataifa yote yatoe ushrikiano unaohitajika wa kuondolewa wapiganaji wa kigeni katika taifa hili. Kwa mtazamo wetu, hili ni jambo linalopaswa kupewa kipaumbele, kwani usalama wetu una mafungamano na kuondoka vikosi hivyo vya kigeni.
Licha ya takwa la sisitizo hilo la viongozi wa Libya, lakini vikosi vya kigeni vimeendelea kuweko nchini humo kwa visingizio mbalimbali . Askari wa Uturuki wanaunda sehemu kubwa ya wanajeshi wa kigeni nchini Libya. Viongozi wa Uturuki wanadai kwamba, askari hao ni sehemu ya makubaliano kwa ajili ya kuwapatia mafunzo askari wa Kilibya ambayo ilitiliana saini na serikali iliyopita ya Tripoli.
Hii ni katika hali ambayo, ukweli wa mambo ni kuwa uwepo wa askari hao sio tu kwamba, unakwamisha mwenendo wa kurejeshwa amani na usalama katika ardhi yote ya Libya, bali hatua hiyo inahesabiwa kuwa tishio kubwa kwa mataifa mengine yanayopakana na nchi hiyo ya kaskazini mwa Afrika.
Ni kwa kuzingatia hilo ndio maana Abdul Hamid Dbeibeh, Waziri Mkuu wa Serikali ya Muda ya Libya akatoa indhari kwa kusema kuwa, askari wa kukodiwa na mamluki wa kigeni ni ‘pigo jambia kwa nyuma’ dhidi ya taifa la Libya ambalo linafanya juhudi za kuikomboa nchi hiyo kutoka katika makucha ya mamluki hao.
Himesh Kinner, mtafiti wa masuala ya kisiasa anasema kuwa, kusambaratishwa wanamgambo wabeba silaha inaonekana kuwa hatua muhimu na ufunguo wa kuleta amani, hata hivyo baadhi yao hawana shauku wala nia ya kuweka chini silaha na hivyo kufumbia macho mamlaka yao ya kujitawala.
Licha ya kuwa, Walibya wana matumaini kwamba, vikosi vya kigeni vilivyoko katika nchi yao vitaondoka haraka katika ardhi ya nchi hiyo na hivyo viongozi wa nchi kuweza kuandaa mazingira ya kufanyika uchaguzi katika tarehe iliyopangwa wakiwa katika anga tulivu kabisa, lakini uwepo wa askari hao bado ni kizuizi kikubwa katika njia ya kufikia lengo hilo. Kuna wasiwasi kwamba, uingiliaji wa kigeni katika masuala ya ndani ya Libya, ukakwamisha utendaji wa serikali ya muda na ya umoja wa kitaifa na hivyo kushindwa kufikia malengo yaliyoainishwa.