Mjumbe wa UN: Mamluki walioko Libya ni tishio kwa Afrika ya Kaskazini
Mjumbe maalumu wa Umoja wa Mataifa nchini Libya ametahadharisha katika kikao cha Baraza la Usalama kwamba mchakato muhimu wa kuwaondoa mamluki na wapiganaji wa kigeni kutoka Libya umekwama na kwamba kuendelea kuwapo kwao nchini humo ni tishio sio tu kwa Libya bali kwa eneo zima la Kaskazini mwa Afrika.
Jan Kubis amesema matukio ya hivi karibuni katika nchi jirani ya Chad, ambapo waasi walilaumiwa kwa mauaji ya mwezi uliopita ya rais wa muda mrefu wa nchi hiyo, Idriss Deby, ni kielelezo cha uhusiano uliopo kati ya hali ya usalama nchini Libya na usalama na utulivu katika eneo hilo.
Kubis amesema: "Harakati kubwa za makundi yenye silaha na magaidi na vilevile wahajiri wa kiuchumi na wakimbizi, ambao mara nyingi hupitia katika njia zinazosimamiwa na mitandao ya wahalifu na wachezaji wengine wa ndani katika mipaka isiyodhibitiwa, zinazidisha hatari za kosefu wa usalama nchini Libya na kanda hiyo nzima."
Amesema ujumbe wa UN nchini Libya unaojulikana kwa jina la UNSMIL, umeripoti "uwepo wa raia wa kigeni, mamluki na zana," ambavyo amesema vinazidisha migawanyiko nchini Libya.
Libya ilitumbukia katika machafuko baada harakati iliyoungwa mkono na NATO kumuondoa madarakani mtawala wa muda mrefu wa nchi hiyo, Muammar Gaddafi mnamo 2011. Machauko hayo yaliigawa nchi hiyo yenye utajiri wa mafuta kati ya sehemu mbili za serikali inayotambuliwa na UN katika mji mkuu, Tripoli, na mamlaka hasimu iliyokuwa uikitawala mashariki mwa nchi hiyo.
Serikali mpya ya umoja wa kitaifa ya Libya inayoongozwa na Waziri Mkuu Abdulhamid al-Dabaiba na Baraza la Urais chini ya uongozi wa Mohamed al-Menfi, tarehe 16 mwezi wa Machi mwaka huu ilishika rasmi hatamu za kuiongoza nchi hiyo na kupewa jukumu la kutayarisha mazingira ya kuitishwa chaguzi za Bunge na Rais mwishoni mwaka huu wa 2021.