Haftar azuiwa kugombea katika uchaguzi ujao wa Libya
Kiongozi wa Baraza Kuu la Libya amepinga suala la wanajeshi kugombea katika uchaguzi ujao wa nchi hiyo akiwemo kamanda wa kundi la wanamgambo wa linalojiita Jeshi la Kitaifa la Libya, Khalif Haftar.
Khalid al Mushiri alisema jana katika mkutano na waandishi wa habari kuwa, haikubaliki wanajeshi kugombea katika chaguzi za bunge na rais zilizopangwa kufayika Disemba 24 mwaka huu nchini Libya akiwemo Khalifa Haftar, kamanda wa kundi la wanamgambo wa Jeshi la Kitaifa la Libya.
Al Mushiri ameongeza kuwa, anapinga kushinikizwa mjumbe wa Umoja wa Mataifa katika masuala ya Libya ili kutoa kibali kwa wanajeshi kugombea katika uchaguzi ujao. Kiongozi wa Baraza Kuu la Libya ameitaja katiba kuwa ni msingi na kigezo cha kuendeshea uchaguzi nchini humo na akasema vizuizi vyote katika uwanja huo vinapasa kuondolewa hadi kufikia tarehe 24 Disemba.
Hii ni katika hali ambayo, mazungumzo ya hivi karibuni kuhusu Libya yaliyofanyika mjini Geneva, Uswisi ambayo yalitazamia kuainisha namna uchaguzi wa rais na bunge wa Libya utakavyofanyika kwa mujibu sheria kabla ya tarehe Mosi mwezi Julai, yalimalizika bila ya natija yoyote.
Wajumbe na maafisa wa Umoja wa Mataifa walioshiriki mazungumzo ya Geneva kuhusu Libya wamesema kuwa wameshindwa kufikia mapatano kuhusu baadhi ya mapendekezo yaliyowasilishwa na suala hilo limewapelekea waandaaji wa kikao hicho kuongeza muda wa mazungumzo.