Watu 19 wauawa katika shambulizi jipya la wabeba silaha Niger
(last modified Fri, 30 Jul 2021 12:39:44 GMT )
Jul 30, 2021 12:39 UTC
  • Watu 19 wauawa katika shambulizi jipya la wabeba silaha Niger

Raia 19 wameuawa kwenye shambulizi linaloaminika kuwa la kigaidi katika mpaka wa Niger na Mali.

Maafisa wa serikali ya Niger wamenukuliwa wakisema hayo jana Alkhamisi na kuongeza kuwa, watu wenye silaha wasiojulikana walishambulia kijiji cha Deye Koukou katika mkoa wa Banibangou magharibi mwa nchi na kuua raia wasiopungua 19.

Habari zaidi zinasema kuwa, watu wengine wanne wamejeruhiwa katika shambulizi hilo. Hadi kufikia sasa hakuna kundi lililotangaza kuhusika na shambulizi hilo.

Haya yanajiri chini ya wiki moja baada ya raia wengine 14 kuuliwa katika shambulio lililofanywa na kundi la wabeba silaha katika mkoa huo huo wa magharibi mwa nchi.

Magenge ya wabeba silaha Niger

Taarifa iliyotolewa na serikali ya Niamey ilieleza kuwa, kundi la watu wenye silaha Jumapili iliyopita lilishambulia eneo la Bani Bango magharibi mwa nchi na kuua raia 14, mbali na mmoja aliyejeruhiwa na kukimbizwa hospitalini.

Maeneo mbali mbali ya Niger yamekuwa yakiandamwa na mashambulio ya mara kwa mara ya umwagaji damu ya makundi ya wabeba silaha yenye mfungamano na mtandao wa kigaidi wa Al Qaeda na kundi la kigaidi na ukufurishaji la DAESH (ISIS).

Tags