Wanajeshi wadai kufanya mapinduzi nchini Guinea Conakry; wamtia mbaroni Rais Alpha Conde
Wanajeshi wa Guinea wamejitokeza katika runinga ya taifa wakithibitisha kwamba rais Alpha Conde ameondolewa madarakani. Hata hivyo Serikali imesema imerejesha hali ya utulivu
Magari ya deraya yalionekana yakizunguka mitaani mchana kutwa hiyo jana, huku maafisa usalama wakilinda doria wakiwa wamejizatiti kwa silaha.
Kwa mujibu wa shika la habari la Reuters, kwa akali watu wawili wamepata majeraha mabaya katika ufyatulianaji wa risasi wa jana Jumapili Haijabainika makabiliano hayo ya risasi karibu na kasri la rais wa nchi hiyo yalikuwa baina ya makundi au vikosi gani.
Hata hivyo baadhi ya vyanzo vya habari vimedokeza kuwa, ghasia za jana ziliibuliwa na kikosi maalumu cha jeshi la taifa, kikiongozwa na Mamady Doumbouya, mwanachama wa zamani wa jeshi la Ufaransa.
Baada ya milio ya risasi kunyamaza, mpambe wa rais wa nchi hiyo alisambaza kipande cha video akisema, "Rais Alpha Conde anaendelea vizuri, hali imeweza kudhibitiwa."
Oktoba mwaka jana, watu 10 waliuawa katika ghasia za baada ya uchaguzi wa rais katika mji huo mkuu wa Guinea, Conakry. Hii ni baada ya Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi ya nchi hiyo kutangaza kuwa Rais Alpha Conde (83) ameibuka mshindi na ataendelea kuhudumu kwa muhula wa tatu.
Kabla ya hapo, Cellou Dalein Diallo, kiongozi wa chama cha upinzani cha Union of Democratic Forces of Guinea (UFDG) alijitangaza mshindi wa uchaguzi huo wa rais, na kuibua taharuki na wasi wasi kwa muda nchini humo.