Mabaki ya ndege ya EgyptAir yapatikana Baharini
Jeshi Wanamaji la Misri limesema kuwa limepata baadhi ya mabaki ya ndege ya abiria ya EgyptAir katika Bahari ya Mediterranean yapata kilomita 290 kaskazini mwa mji wa pwani wa Alexandria.
Msemaji wa jeshi hilo Mohamed Samir amesema, ndege ya Misri na meli za kijeshi zimepata baadhi ya mizigo ya abiria na mabaki ya ndege hiyo, na kwamba juhudi za kutafuta mabaki ya ndege hiyo baharini zinaendelea.
Wizara ya usafiri wa anga ya Misri imesema, nchi hiyo, Ugiriki na Ufaransa zinashirikiana katika kuitafuta ndege hiyo.
Ndege aina ya Airbus A320 ilipotea kwenye rada wakati ikitokea Paris kuelekea Cairo hapo jana, ikiwa na abiria 66 ndani, wakiwemo raia 30 wa Misri na 15 wa Ufaransa.
Kwingineko Sherif Ismail Waziri Mkuu wa Misri amesema kuwa, kuna uwezekano kutoweka kwa ndege ya nchi hiyo kukawa kumetokana na operesheni ya kigaidi.