Mpango wa maridhiano ya kitaifa nchini Libya
Mkuu wa Baraza la Uongozi nchini Libya Mohamed al-Menfi ametangaza kwamba mpango wa maridhiano ya kitaifa umeanza rasmi nchini humo na kwamba utekelezaji wa mpango huo ni hatua muhimu katika njia ya kukomesha machafuko katika nchi hiyo ya kaskazini mwa Afrika.
Mashauriano ya kumaliza mgogoro wa ndani nchini Libya yanaendelea kwa miezi kadhaa yakishirikisha wawakilishi wa vyama na makundi ya kisiasa, wajumbe wa nchi za kigeni na mjumbe maalumu wa Umoja wa Mataifa katika masuala ya Libya. Miongoni mwa masuala yaliyojadiliwa katika mashauriano hayo ni pamoja na jinsi ya kuitisha na kufanyika uchaguzi wa tarehe 24 Disemba, njia za kusuluhisha hitilafu zilizopo baina ya makundi na vyama vya siasa, na kubuni sheria za baada ya uchaguzi wa rais.
Mapatano yaliyofikiwa katika vikao na mashauri hayo yamerejesha hali ya utulivu wa kiwango fulani nchini Libya. Hata hivyo kuwepo kwa wapiganaji wa kigeni na uingiliaji kati wa nchi za nje bado vinatambuliwa kuwa vizingiti vikubwa katika njia ya kurejesha amani kamili katika nchi hiyo yenye utajiri wa mafuta ya kaskazini mwa Afrika. Hivyo, miongoni mwa masuala muhimu yanayojadiliwa kwa sasa ni pamoja na kadhia ya kuwafukuza mamluki, wapiganaji na majeshi ya nchi za kigeni katika ardhi ya Libya na kukata mirija ya madola ya kigeni nchini humo. Katika mkondo huo, kikao cha mataifa jirani na Libya kilichofanyika nchini Algeria kimesisitiza ulazima wa kuzuia kupatiwa silaha mamluki na wakati huo huo kukabiliana na hatua za kuzusha mifarakano miongoni mwa Walibya. Kikao cha Mawaziri wa Mashauri ya Kigeni wa mataifa 6 jirani na Libya kimesisitiza katika taarifa yake mwishoni kwamba, wamekubaliana kutuma ujumbe maalumu wa kutathmini mwenendo wa kisiasa nchini Libya kabla ya kufanyika uchaguzi mkuu.
Aidha mawaziri hao wamesisitiza udharura wa kuondoka majeshi yote ya kigeni pamoja na mamluki waliopo Libya na kushirikishwa mataifa jirani katika mchakato wa kuikarabati nchi hiyo iliyoharibiwa na vita.
Juhudi hizo za kuwafukuza wapiganaji na majeshi ya kigeni nchini Libya zinafanyika sambamba na mkakati wa kutayarisha mazingira bora ya kuitishwa uchaguzi mkuu mwishoni mwa mwaka huu. Katika mkondo huo siku za karibuni serikali ya mpito ya Libya imewaachia huru wafungwa kadhaa wakiwemo maafisa wa kisiasa wa utawala wa zamani wa nchi hiyo kama Ahmad Ramadhan aliyekuwa Katibu Muhtasi wa kiongozi wa zamani wa Libya, Muammar Gaddafi na vilevile mtoto wake wa tatu, Saadi Gaddafi.
Ofisi ya mjumbe maalumu wa Umoja wa Mataifa nchini Libya imepongeza hatua hiyo ya kuachiwa huru maafisa wa utawala wa zamani wa Libya na kusema ni hatua muhimu ya kuelekea kwenye utawala wa sheria, kuheshimu haki za binadamu na mabadiliko chanya yanayoweza kuchangia katika mchakato wa kuimarisha umoja wa kitaifa katika nchi hiyo.
Inaonekana kuwa makundi ya kisiasa ya Libya yameazimia ipasavyo kutupilia mbali hitilafu zao na kurejesha amani na utulivu kupitia njia ya mwafaka na maridhiao ya kitaifa. Hata hivyo suala hilo halitatimia isipokuw baada ya kufukuzwa mamluki na wapiganaji wote wa kigeni katika ardhi ya Libya na kukatwa kikamilifu mikono ya madola ya kigeni yanayotaka kung'ang'ania na kupora utajiiri wa nchi hiyo kupitia njia ya kuzusha hitilafu na mifarakano baina ya makundi ya kikaumu na vyama mbalimbali vya siasa.