Bunge la Libya lapitisha sheria ya uchaguzi wa rais uliopangwa kufanyika Desemba
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i74494-bunge_la_libya_lapitisha_sheria_ya_uchaguzi_wa_rais_uliopangwa_kufanyika_desemba
Duru za habari zimetangza kuwa bunge la Libya limepitisha sheria ya uchaguzi wa rais uliopangwa kufanyika mwezi Desemba mwaka huu.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Sep 10, 2021 08:03 UTC
  • Bunge la Libya lapitisha sheria ya uchaguzi wa rais uliopangwa kufanyika Desemba

Duru za habari zimetangza kuwa bunge la Libya limepitisha sheria ya uchaguzi wa rais uliopangwa kufanyika mwezi Desemba mwaka huu.

Bunge la Libya limetangaza kuwa spika wa bunge hilo Aqilah Saleh Issa amesaini hati rasmi ya sheria ya uchaguzi wa rais wa nchi hiyo.

Kwa mujibu wa tangazo la bunge, Saleh ametuma nakala za sheria hiyo kwa taasisi nyingine za kisiasa pamoja na Umoja wa Mataifa.

Kwa mujibu wa ripoti za duru hizo za habari, spika wa bunge la Libya amesaini hati hiyo rasmi ya sheria ya uchaguzi wa rais wakati baraza kuu la serikali ya nchi hiyo limeipinga hati hiyo.

Taarifa iliyotolewa na baraza hilo sambamba na kupitishwa na bunge sheria ya uchaguzi wa rais imesema: "Saleh amepitisha makusudi sheria pungufu ya uchaguzi kwa kutaka kukwamisha na kuweka vizuizi katika uendeshaji wa uchaguzi ujao."

Spika wa Bunge la Libya  Aqilah Saleh Issa

Sheria hiyo mpya ya uchaguzi wa rais wa Libya inatoa ruhusa kwa maafisa wanaohudumu hivi sasa kugombea katika uchaguzi huo kwa sharti la kujiuzulu kwa muda nyadhifa zao, miezi mitatu kabla ya tarehe ya uchaguzi huo, ambao umepangwa kufanyika Desemba 24.

Libya iligubikwa na machafuko, vita na mapigano tangu lilipoanza vuguvugu la mapambano ya wananchi mwaka 2011 lililopelekea kuangushwa utawala wa kiongozi wa zamani wa nchi hiyo Muammar Gaddafi, sambamba na uingiliaji uliofanywa na Marekani na baadhi ya nchi za Ulaya na eneo.../