Waasi washambulia gereza Nigeria, zaidi ya mahabusu 800 watoroka
Idara ya Magereza ya Nigeria imetangaza kuwa watu waliokuwa wamejizatiti kwa silaha wameshambulia magereza moja huko kusini magharibi mwa nchi hiyo na kuachia huru mahabusu 837.
Afisa wa Mawasiliano ya Umma wa Gereza la Abolongo, Olanrewaju Anjorin amesema kuwa waasi hao walivamia gereza hilo Ijumaa iliyopita kwa kutumia maguruneti.
Anjorin amesema mahabusu wote 837 waliokuwa wakisubiri kesi zao waliachiwa huru na kwamba 262 kati yao wamekatwa na kurejeshwa mahabusu na kwamba 575 hawajulikani waliko.
Amesema operesheni ya kuwasaka na kuwarejesha mahabusu bado inaendelea.
Kituo hicho chenye uwezo wa kuhifadhi mahabusu 160 tu kilikuwa na wafungwa 907 wakati wa shambulizi hilo.
Waasi na makundi ya magaidi wenye silaha wamekuwa wakishambulia magereza na ofisi za umma nchini Nigeria katika miezi ya karibuni.
Wafungwa wasiopungua 3,590 wametoroka katika mashambulio mblimbali yaliyofanyika katika mji wa Owerri katika jimbo la Imo.