Afrika Kusini 'yamnawa' raia wake atakayeshiriki tamasha la ulimbwende Israel
Serikali ya Pretoria imejibari na uamuzi wa 'Bi Afrika Kusini' Lalela Mswane wa kukubali mwaliko wa kushiriki Tamasha la Ulimbwende linalotazamiwa kufanyika mwezi ujao huko Israel.
Waziri wa Utamduni na Sanaa wa Afrika Kusini, Nathi Mthethwa amesema serikali imejaribu kumshawishi mwanamke huyo ambaye hivi karibuni alivikwa taji la kuwa mwanamke mrembo zaidi nchini humo, asishiriki katika shughuli hiyo inayoandaliwa na Israel, lakini mwito wao ukaangukia sikio la kufa.
Amesema serikali ya Afrika Kusini haitahusika kivyovyote na maandalizi au ushiriki wa mwanamke huyo katika tamasha hilo la urembo linalotazamiwa kufanyika Disemba 12 katika mji wa Eilat, huko Palestina inayokaliwa kwa mabavu na Israel.
Waziri huyo ameonya kuwa, kushiriki kwa mwanadada huyo kwenye mashindano hayo ya Israel sanjari na kupuuza mwito wa wananchi walio wengi, kutamponza Bi Afrika Kusini katika mustakabali wake, na kubadilisha namna jamii inavyomtazama kama mwanamke mchanga wa Kiafrika.
Wizara ya Utamaduni na Sanaa ya Afrika Kusini imesisitiza kuwa, "jinai zinazofanywa na Israel dhidi ya Wapalestina ziko wazi na serikali (ya Afrika Kusini) kama mwakilishi halali wa Waafrika Kusini haiwezi kujihusisha na shughuli hiyo."
Afrika Kusini imekuwa ikionyesha wazi wazi msimamo wake wa kupinga jinai zinazofanywa na utawala wa Kizayuni wa Israel dhidi ya wananchi madhulumu wa Palestina kwa miaka mingi sasa.
Julai mwaka huu, nchi hiyo ilipinga kitendo cha kutambuliwa utawala haramu wa Israel kuwa mwanachama mtazamaji wa Umoja wa Afrika (AU) na kusisitiza kuwa, uamuzi huo si wa kiadilifu na wala hauwezi kuhalalishwa kwa njia yoyote ile.