Walibya waandamana wakipinga kukubaliwa Saiful Islam Gaddafi kugombea urais
-
Saiful Islam Gaddafi
Raia wa maeneo ya magharibi mwa Libya wamefunga vituo vya kupigia kura wakipinga hatua ya mwana wa kiume wa kiongozi wa zamani wa Libya, Saiful Islam Gaddafi ya kuwania kiti cha urais katika uchaguzi ujao nchini humo.
Hahari zinasema raia wa maeneo hayo wamevamia na kufunga vituo vya kupigia kura katika miji ya Gharyan na Zliten na kwamba Tume ya Uchaguzi Libya pia imefunga ofisi yake katika mji wa Al-Khums kutekeleza matakwa ya wakazi wa mji huo.
Maandamano ya kupinga hatua ya Saiful Islam Gaddafi kujiandikisha kwa ajili ya kugombea kiti cha rais wa Libya pia yameshuhudiwa katika mji wa Misrata ambako waandamanaji wamelaani hatua ya Tume ya Uchaguzi Libya ya kukubali hati za kugombea za Saiful Islam.
Katika upande mwingine ofisi ya Mwendesha Mashtaka Mkuu wa Kijeshi nchini Libya ameitaka Tume ya Uchaguzi Libya isitishe maombi ya Saiful Islam Gaddafi na jenerali mstaafu Khalifa Haftar ya kutaka kugombea kiti cha rais wa nchi hiyo katika uchaguzi ujao.
Taarifa iliyotolewa na ofisi hiyo imesema maombi ya wawili hao ya kugombea urais yanapaswa kusitishwa hadi baada ya kufanyiwa uchunguzi.
Saiful Islam Gaddafi, mwana wa kiume wa kiongozi wa zamani wa Libya, Kanali Muammar Gaddafi, alitangaza rasmi azma yake ya kugombea urais katika nchi hiyo ya kaskazini mwa Afrika Jumapili iliyopita.
Saiful Islam ni wa pili kujiandikisha rasmi kwa ajili ya uchaguzi huo uliopangwa kufanyika mwishoni mwa mwaka huu.
Awali Tume ya Uchaguzi Libya ilikuwa imetangaza kwamba ofisi yake katika mji mkuu, Tripoli, imepokea nyaraka za maombi za Abdel Hakim Bayou kama faili la kwanza kwa mgombea urais.
Wengine wanaotazamiwa kujitosa katika kinyang'anyiro hicho ni kamanda muasi wa jeshi jenerali Khalifa Haftar, Waziri Mkuu wa sasa wa Libya Abdulhamid al-Dbeibah na Spika wa Bunge Aguila Saleh.