Jenerali Haftar, ajenti wa zamani wa CIA atangaza kugombea urais wa Libya
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i76990-jenerali_haftar_ajenti_wa_zamani_wa_cia_atangaza_kugombea_urais_wa_libya
Khalifa Haftar, kamanda wa kundi linalojiita Jeshi la Taifa la Libya (LNA) ametangaza kuwa atagombea urais wa nchi hiyo katika uchaguzi uliopangwa kufanyika mwezi ujao wa Desemba.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Nov 17, 2021 03:01 UTC
  • Jenerali Haftar, ajenti wa zamani wa CIA atangaza kugombea urais wa Libya

Khalifa Haftar, kamanda wa kundi linalojiita Jeshi la Taifa la Libya (LNA) ametangaza kuwa atagombea urais wa nchi hiyo katika uchaguzi uliopangwa kufanyika mwezi ujao wa Desemba.

Akitangaza azma yake hiyo katika hotuba aliyotoa kwa njia ya televisheni, Haftar amesema, "chaguzi ndio njia pekee ya kuitoa nchi yetu kwenye lindi la mgogoro mbaya iliotumbukia ndani yake."

Kamanda huyo wa kundi la LNA lenye makao yake mashariki ya Libya alianzisha vita dhidi ya mirengo ya magharibi, baada ya nchi hiyo kugawanyika pande mbili mwaka 2014, ikiwemo operesheni kali ya kijeshi miezi 14 iliyolenga kuuteka mji mkuu Tripoli, lakini ikazimwa na vikosi vya serikali iliyokuwa ikitambuliwa na jamii ya kimataifa.

Khalifa Haftar, ambaye ni shakhsia mtatanishi aliyewahi kuwa ajenti wa Shirika la Ujasusi la Marekani, CIA anaungwa mkono na Russia, Misri na Imarati.

Uamuzi wa jenerali huyo mwasi wa jeshi la Libya wa kugombea urais utawakasirisha watu wengi katika mji mkuu Tripoli na maeneo ya magharibi mwa nchi, ambao wanaamini upigaji kura utakaofanyka katika maeneo yanayodhibitiwa na kundi lake la LNA hautakuwa huru na wa haki. 

Wapinzani wake hao wanamtuhumu pia kuhusika na jinai za kivita wakati wa mashambulio aliyoongoza dhidi ya serikali ya Tripoli, madai ambayo, Haftar mwenyewe anayakanusha.

Tarehe 22 Septemba, Jenerali Haftar alitangaza kustaafu cheo chake cha uongozi wa kundi la LNA kama sheria inavyomtaka ili aruhusike kugombea urais.

Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi ya Libya Imad Saayih ametangaza kuwa uandikishaji wa wagombea ubunge utaendelea hadi tarehe 7 ya mwezi ujao wa Desemba na wa wagombea urais hadi tarehe 22 ya mwezi huu wa Novemba. 

Uchaguzi wa rais na bunge wa Libya unatazamiwa kufanyika tarehe 24 Desemba.../