Idara ya uchunguzi wa vifo: Mripuko ulitokea ndani ya ndege ya Egyptair
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i7762-idara_ya_uchunguzi_wa_vifo_mripuko_ulitokea_ndani_ya_ndege_ya_egyptair
Afisa wa Idara ya uchunguzi wa vifo ya Misri ametangaza kuwa mabaki ya viwiliwili vya watu waliofariki kwenye ajali ya ndege ya shirika la ndege la nchi hiyo yanaonesha kuwa ulitokea mripuko ndani ya ndege hiyo kabla ya kuanguka katika Bahari ya Mediterania.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
May 24, 2016 23:38 UTC
  • Idara ya uchunguzi wa vifo: Mripuko ulitokea ndani ya ndege ya Egyptair

Afisa wa Idara ya uchunguzi wa vifo ya Misri ametangaza kuwa mabaki ya viwiliwili vya watu waliofariki kwenye ajali ya ndege ya shirika la ndege la nchi hiyo yanaonesha kuwa ulitokea mripuko ndani ya ndege hiyo kabla ya kuanguka katika Bahari ya Mediterania.

Afisha huyo ameongeza kuwa hadi sasa hayajapatikana mabaki au athari ya mada za miripuko lakini uchunguzi wa awali uliofanywa katika mabaki ya viwiliwili vya watu waliofariki kwenye ajali hiyo umezidi kuupa nguvu uwezekano kwamba mripuko ulitokea ndani ya ndege hiyo.

Hata hivyo shirika la habari la Reuters limemnukuu afisa mwengine wa Idara ya uchunguzi wa vifo ya Misri akisema kuwa ni idadi ndogo ya mabaki ya viwiliwili vya waliofariki kwenye ajali hiyo ya ndege iliyopatikana hadi sasa na kupelekwa nchini humo na kwamba ni mapema kutoa uamuzi kuwa mripuko ulitokea ndani ya ndege hiyo.

Awali ilikuwa imetangazwa kwamba taarifa za ndege hiyo zimeonesha kuwa baadhi ya sehemu za ndege kikiwemo choo na baadhi ya vifaa vya elektroniki viljaa moshi dakika chache kabla ya ndege hiyo kuanguka.

Aidha siku ilipotokea ajali hiyo baadhi ya vyombo vya habari vya nchi za Kiarabu viliwanukuu mashuhuda katika kisiwa kimoja nchini Ugiriki wakisema kuwa ilionekana ndege angani iliyokuwa ikiwaka moto.

Ndege aina ya Airbus A320 ya shirika la ndege la Misri ilianguka siku ya Alhamisi katika Bahari ya Mediterania wakati ikitokea Paris, Ufaransa kuelekea Cairo, Misri ikiwa na jumla ya wasafiri 66. Watu wote waliokuwamo ndani yake walifariki dunia.../