Afrika Kusini yajiandaa kukabiliana na kesi zaidi za maambukizi ya Omicron
-
Cyril Ramaphosa,
Rais wa Afrika Kusini, Cyril Ramaphosa, amesema hospitali za nchi hiyo zinajiandaa kwa ajili ya kupokea wagonjwa zaidi wa virusi vya corona huku nchi hiyo ikiingia kwenye wimbi la nne la maambukizi ya COVID-19 hususan aina ya mpya ya kirusi cha Omicron.
Ramaphosa alisema jana Jumatatu kwamba: "Nchi inapoelekea katika wimbi la nne la maambukizo ya COVID-19, tunapitia kiwango kikubwa cha maambukizi ambacho hakijawahi kushuhudiwa tangu janga hili lianze."
Omicron aligunduliwa nchini Afrika Kusini mwezi uliopita na kusababisha wasiwasi wa kimataifa huku kukiwa na hofu ya kuongezeka kwa maambukizi mapya.
Maambukizi ya kila siku ya kesi za COVID-19 nchini Afrika Kusini yaliongezeka wiki iliyopita hadi zaidi ya 16,000 siku ya Ijumaa pekee, kutoka takriban 2,300.
Rais Ramaphosa amesema kwamba, Omicron inaonekana kutawala kesi mpya za maambukizi ya corona katika majimbo tisa ya nchi hiyo na amewataka watu kupata chanjo dhidi ya COVID-19.

Amesema chanjo ni muhimu kwa ajili ya kufufua uchumi wa Afrika Kusini kwa sababu kadiri watu wengi zaidi wanavyochanjwa ndivyo maeneo mengi ya shughuli za kiuchumi yanavyofunguliwa.
Wanasayansi nchini Afrika Kusini na nchi nyingine duniani wanafanya juhudi kubwa za kubaini iwapo kirusi cha corona aina ya Omicron kinaambukiza zaidi, kusababisha ugonjwa mbaya zaidi na kama ni sugu kwa chanjo zilizopo za corona au la.
Hadi sasa kirusi hicho kimeripotiwa katika nchi zaidi ya 45 duniani ingawa ripoti za awali zinasema, inaonekana kuwa aina hii ya corona si hatari zaidi ya ile ya awali ya Delta.