EU yatakiwa iache kuiuzia silaha Misri ili kukomesha mauaji na ukandamizaji
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i7780-eu_yatakiwa_iache_kuiuzia_silaha_misri_ili_kukomesha_mauaji_na_ukandamizaji
Shirika la kutetea haki za binadamu la Amnesty International limeutaka Umoja wa Ulaya uache kuiuzia silaha na zana za kijeshi Misri na kusisitiza kuwa umoja huo unaisadia serikali ya Cairo katika mauaji na ukandamizaji wa raia.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
May 25, 2016 03:01 UTC
  • EU yatakiwa iache kuiuzia silaha Misri ili kukomesha mauaji na ukandamizaji

Shirika la kutetea haki za binadamu la Amnesty International limeutaka Umoja wa Ulaya uache kuiuzia silaha na zana za kijeshi Misri na kusisitiza kuwa umoja huo unaisadia serikali ya Cairo katika mauaji na ukandamizaji wa raia.

Katika taarifa liliyotoa leo, shirika hilo la Msamaha Duniani limesema, nchi 12 wanachama wa Umoja wa Ulaya zikiwemo Uingereza, Ufaransa, Ujerumani na Italia pamoja na Bulgaria na Jamhuri ya Czech zimeendelea kuwa wauzaji wa silaha na vifaa vya jeshi la Polisi kwa serikali ya Misri na kufafanua kuwa nchi hizo zimekiuka mpango mpana wa EU wa kusimamisha uuzaji silaha kwa Misri uliotekelezwa baada ya mauaji ya mamia ya waandamanaji kupitia kile kilichoelezwa kuwa ni "utumiaji nguvu kupindukia" wa mwezi Agosti mwaka 2013.

Kwa mujibu wa Magdalena Mughrabi, Naibu Mkurugenzi wa Amnesty International katika kanda ya Mashariki ya Kati na Kaskazini mwa Afrika, hali ya haki za binadamu nchini Misri imezidi kuwa mbaya.

Amnesty imeripoti kuwa katika mwaka 2014 pekee nchi za Umoja wa Ulaya ziliidhinisha vibali 290 vya mauzo ya zana za kijeshi kwa Misri zenye thamani ya zaidi ya yuro bilioni sita.

Shirika hilo la kutetea haki za binadamu aidha limemtuhumu Rais Abdel Fattah el Sisi wa Misri kuwa anaendesha utawala kidikteta na kwa ukandamizaji mkubwa tangu Muhammd Morsi, rais aliyechaguliwa kidemokrasia na wananchi alipoondolewa madarakani mwaka 2013 kupitia mapinduzi ya kijeshi yaliyoongozwa na el Sisi.../