Kuendelea mivutano ya uchaguzi huko Libya
(last modified Mon, 13 Dec 2021 04:30:02 GMT )
Dec 13, 2021 04:30 UTC
  • Kuendelea mivutano ya uchaguzi huko Libya

Katika kipindi hiki cha kukaribia wakati wa kufanyika uchaguzi huko Libya, mivutano ya kisiasa imepamba moto nchini humo kwa kadiri kwamba, Tume Kuu ya Uchaguzi ya nchi hiyo imetangaza habari kuakhirishwa zoezi la kuchapisha orodha ya mwisho ya wagombea wa kiti cha urais.

Uchaguzi wa Rais wa Libya umepangwa kufanyika tarehe 24 mwezi huu wa Disemba; hata hivyo ukwamishaji wa hapa na pale unaendelea kushuhudiwa katika mchakato wa zoezi hilo zikiwa zimesalia wiki mbili mbili tu hadi kufanyika uchaguzi huo. Awali Omar Abdel Aziz Bushah Naibu Mkuu wa Baraza Kuu la Uongozi la Serikali ya Umoja wa Kitaifa ya Libya alitoa pendekezo la kuakhirishwa uchaguzi huo. Bushah alitoa wito  kuakhirishwa uchaguzi wa rais wa Libya hadi Februari mwaka ujao wa 2022 badala ya Disemba 24 mwaka huu.  

Licha ya mazungumzo na juhudi za kisiasa yaliyofanyika hadi sasa kwa ajili ya kutafuta suluhisho la mgogoro wa Libya, laikini inaonekana kuwa nchi hiyo inasumbuliwa na matatizo makubwa mawili, ambayo ni kuendelea hitilafu za ndani na kuongezeka uingiliaji wa nchi ajinabi katika masuala ya Libya.  

Omar Bushah Naibu Mkuu wa Baraza Kuu la Uongozi Libya ameshiria mivutano ya kisiasa na kutoaminiana kati ya vyama na makundi ya Libya na vilevile uingiliaji wa nchi ajinabi katika masuala ya ndani ya nchi hiyo na kueleza kuwa "hali inayoendelea kushuhudiwa hivi sasa nchini Libya inatishia mchakato wa kisiasa."   

Omar Bushah, Naibu Mkuu wa Baraza Kuu la Uongozi Libya 

Hitilafu za ndani huko Libya zimezuia watu wengi kugombea katika uchaguzi ujao wa nchi hiyo. Hatua ya Saiful Islam Gaddafi, mwana wa kiume wa kiongozi wa zamani wa nchi hiyo, Kanali Muammar Gaddafi na Jenerali Khalifa Haftar kujiandikisha kwa ajili ya kugombea katika uchaguzi ujao imezidisha mivutano ya kisiasa nchini Libya. Saiful Islam Gaddafi anasakwa na Mahakama ya Kimataifa ya Jinai (ICC) kwa tuhuma za kutenda jinai dhidi ya binadamu Vilevile Ofisi ya Mwendesha Mashtaka Mkuu wa Kijeshi ya Libya iliagiza kutiwa nguvuni Saiful Islam kwa kuhusika na mauaji na kuwatumia mamluki katika vita. Hata hivyo Mahakama ya Rufaa katika mji wa Sabha hivi karibuni iliitisha kikao maalumu kuchunguza malalamiko ya Saiful Islam Gaddafi kuhusu kuzuiwa kushiriki katika uchaguzi wa rais na ikatoa dikrii na kutangaza kuwa, Saiful Islam anaweza kushiriki katika uchaguzi bila kizuizi chochote. Suala hilo limechochea mivutano na misuguano huko Libya. Akthari ya wananchi wa Libya wanaamini kuwa, mwana huyo wa kiume wa Gaddafi hafai kuwa mgombea katika uchaguzi wa rais. 

Saiful Islam Gaddafi

Suala la Khalifa Haftar kugombea kiti cha rais katika uchaguzi huo ni suala jingine ambalo limezidisha mivutano nchini Libya. Itakumbukwa kuwa Mahakama ya Rufaa ya Tripoli imepinga na kubatilisha uamuzi uliotolewa na Mahakama ya Mwanzo ya Zawiya uliokuwa umemzuia Khalifa Haftar, kamanda wa wanamgambo wanaojiita jeshi la kitaifa la Libya mashariki mwa nchi hiyo, kugombea katika uchaguzi ujao. Mahakama hiyo imetoa uamuzi kuwa Haftar arejeshewe haki ya kuwania kiti cha urais katika uchaguzi wa Disemba 24. 

Abdulhamid Dbeibeh, Khalifa Haftar, Aguilah Saleh na Saiful Islam Gaddafi ni kati ya shakhsia wanaotazamiwa kugombea kiti cha rais katika uchaguzi wa Libya.  

Aguilah Saleh, ametambuliwa pia kama mgombea wa kiti cha urais Libya 

Wakati huo huo uingiliaji wa nchi za nje katika masuala ya ndani ya Libya pia umeongezeka zaidi hususan katika kipindi hiki cha kukaribia zoezi la uchaguzi mkuu. Inaonekana kuwa nchi mbalimbali zinawania kuwa na ushawishi nchini Libya kupitia njia ya kuwaunga mkono wagombea mbalimbali na zinafanya jitihada za kuhakikisha kuwa zoezi hilo linaakhirishwa. Kuhusiaja na suala hilo mtandao wa Al Arabi al Jadid umefichua mashinikizo ya nyuma ya pazia yanayofanyika katika ngazi mbalimbali za ndani na nje kwa lengo la kuakhirisha uchaguzi huo wa rais uliopangwa kufanyika tarehe 24 mwezi huu wa Disemba. 

Tume ya Taifa ya Uchaguzi Libya imetangaza kuwa itachapisha orodha ya majina ya wagombea wa uchaguzi wa rais  baada ya kutatuliwa matatizo ya kisheria na kuondolewa vizuizi vyote. Kwa utaratibu huo, si jambo lililo mbali uchaguzi wa rais Libya ukashindwa kufanyika kama ilivyopangwa hapo tarehe 24 Disemba.