Aliyechoma moto Bunge la Afrika Kusini kuhukumiwa Februari 4
Zandile Mafe atajua hatima yake siku chache zijazo baada ya mahakama ya jimbo la Cape Town nchini Afrika Kusini kueleza kuwa itatoa hukumu kuhusu mtuhumiwa huyo tarehe 4 mwezi ujao wa Februari. Zandile Mafe anakabiliwa na tuhuma za kuchoma kwa makusudi jengo la Bunge la Afrika Kusini
Hii ni baada ya kusikilizwa kesi hiyo juzi Jumamosi ambapo Mafe aliomba aachiwe huru kwa dhamana baada ya kutiwa nguvuni akituhumiwa kuchoma moto jengo la bunge.
Meryyn Menigo Mwendesha Mashtaka wa serikali ya Afrika Kusini amesema Mafe hapasi kupewa dhamana kwa sababu mtuhumiwa huyo ana kesi kubwa ya kujibu mbele ya Jamhuri. Amesema tuhuma zinazomkabili Mafe ni nzito na zenye mashiko na ushahidi.
Mwendesha Mashtaka wa serikali ya Afrika Kusini amesema kuwa Zandile Mafe alitoa mafuta ya petroli katika gereji moja huko Bellville na kisha akayatumia kuchoma moto jengo la Bunge. Amesema mkanda wa video pia unamuonyesha Mafe akitekeleza hujuma hiyo.
Kwa upande wake Dali Mpofu wakili anayemtetea mtuhumiwa huyo amesema kuwa Jamhuri haina kesi dhidi ya mteja wake. Ameongeza kuwa Mafe anapasa kutambuliwa kama mtu asiye na hatia hadi hapo kosa lake litakapothibitishwa mahakamani.
Mahakama katika jimbo la Cape Town imetangaza kuwa, itatoa hukumu kwa Zandile Mafe Ijumaa ijayo. Itakumbukuwa kuwa moto mkubwa ulizuka mapema mwezi Januari mwaka huu na kuteketeza kikamilifu jengo la Bunge huko Cape Town Afrika Kusini.