May 29, 2016 03:52 UTC
  • Ombi la kufanyika mazungumzo mapana nchini Burundi

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa ametaka kufanyika mazungumzo mapana kati ya wapinzani na serikali ya Burundi.

Ban Ki-moon Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa jana Ijumaa alizitolea wito pande husika katika mgogoro wa Burundi kufanya mazungumzo mapana na vile vile kukaribisha uamuzi wa mpatanishi wa kieneo wa kukutana na wapinzani wa Burundi katika siku chache zijazo.

Ban Ki-moon pia amepongeza jitihada za Benjamin William Mkapa Rais mstaafu wa Tanzania kwa kufanikisha mazungumzo kati ya pande hasimu za Burundi kuanzia tarehe 21 hadi 24 mwezi huu huko Arusha Tanzania.

Benjamin William Mkapa mpatanishi mpya katika mgogoro wa Burundi pia amesema kuwa amepanga kufanya mazungumzo muhimu na makundi ya upinzani Burundi katika muda wa wiki mbili zijazo. Itakumbukwa kuwa makundi hayo yalikataa kushiriki mazungumzo ya Arusha.

Hatua ya Rais Pierre Nkurunziza ya kuwania kiti cha urais kwa muhula wa tatu ambapo kwa mujibu wa wapinzani ni kinyume na katiba, imeitumbukiza Burundi katika mgogoro wa kisiasa tangu mwezi Aprili mwaka jana.

Kuongezeka ghasia na machafuko huko Burundi hadi sasa kumeitia wasiwasi mkubwa jamii ya kimataifa khususan nchi jirani za eneo juu ya uwezekano wa kutokea vita vya ndani nchini humo. Licha ya kutekelezwa jitihada mbalimbali kwa minajili ya kurejesha amani na kufanyika mazungumzo kati ya wapinzani na chama tawala huko Burundi, lakini hakuna natija yoyote iliyopatikana. Rais mstaafu wa Tanzania amechukua nafasi ya upatanishi katika mgogoro wa Burundi huku makundi yenye silaha yakiendeleza mauaji dhidi ya watu wa nchi hiyo. Hapo jana watu wenye silaha wasiofahamika waliishambulia ofisi ya chama tawala katika eneo la Nadawa huko Muaru na kumuua polisi mmoja na kumjeuhi raia mwingine.

Mauaji hayo yameongezeka katika wiki za hivi karibuni kiasi kwamba Farhan Haq MSemaji wa Umoja wa Mataifa wiki iliyopita alitahadharisha kuhusu kuongezeka ghasia na wimbi jipya la utiaji mbaroni wapinzani huko Burundi.

pamoja na hali hii, mazungumzo kuhusu mzozo wa nchi hiyo yalifanyika tarehe 21 hadi 24 za mwezi huu nchini Tanzania kwa kuhudhuriwa na viongozi wa Jumuiya ya Nchi za Afrika Mashariki pamoja na Burundi yenyewe lakini bila ya kuhudhuriwa na muungano mkuu wa upinzani.

Hii ni mara ya tatu ambapo mazungumzo ya kusaka amani Burundi yanafanyika. Mwaka uliopita wa 2015 Rais Yoweri Museveni wa Uganda alijaribu kufanya jitihada katika uwanja huo, hata hivyo jitihada hizo hazikuzaa matunda. Mazungumo ya hivi sasa ya Burundi yamefanyika katika mazingira ya mivutano ya kisiasa ambapo wapinzani wameyataja kuwa yasiyo na itibari yoyote.

Pamoja na hayo yote, Benjamini Mkapa mpatanishi wa mgogoro wa Burundi amesema kuwa

atafanya mazungumzo na makundi yote ya nchi hiyo wakiwemo watu ambao hawakushiriki kikao cha Arusha. Hata kama kuanza tena mazungumzo na kutekelezwa jitihada za kurejesha amani na uthabiti huko Burundi kumeleta matumaini ya kupatiwa ufumbuzi tatizo lililopo, lakini weledi wa mambo wanaamini kuwa ni vigumu mno kupatiwa suluhisho mgogoro wa nchi hiyo kwa njia ya kisiasa bila ya pande mbili hasimu kulegeza misimamo yao. Wapinzani kwa upande wao wanasisitiza kujiuzulu Rais Nkurunziza huku wakiamini kuwa kuwepo kwake madarakani ni kinyume cha sheria. Suala lingine linaloitatiza Burundi mbali na vita hivyo vya kuwania madaraka, ni kuwepo silaha zilizotapakaa miongoni mwa makundi yanayounga mkono na yale yanayopinga kuwepo madarakani Rais Nkurunziza. Inaonekana kuwa kuanza duru hii mpya ya mazungumzo kunahesabiwa kuwa ni juhudi mpya kwa minajili ya kuhitimisha mgogoro wa kisiasa ulioigubika Burundi na kuzuia kujiri vita vingine katika eneo kwa sharti kuwa, makundi yanayoafiki na yale yanayopinga yajongee kwenye meza ya mazungumzo na kufikia makubaliano ili kuhitimisha machafuko nchini humo.

Tags