Burundi yafunga mpaka wake na Rwanda baada ya shambulio la waasi
Burundi imetangaza kuwa imefunga mpaka wake na Rwanda kuanzia jana Alkhamisi kwa muda usiojulikana.
Burundi inamshutumu jirani yake huyo kwamba anapuuza hali ya kuvurugika kwa usalama hususan mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo DRC.
Wiki mbili zilizopita, Burundi iliituhumu Rwanda kuwa inawaunga mkono waasi waliofanya mashambulizi katika ardhi yake, madai ambayo Rwanda iliyakanusha.
Jana Alkhamisi, Waziri wa Mambo ya Ndani wa Burundi Martin Niteretse alithibitisha kuwa mpaka huo umefungwa baada ya wasafiri kuzuiwa kuondoka au kuingia Burundi katika eneo la kaskazini mwa nchi hiyo.
Niteretse alitangaza uamuzi huo wa serikali ya Bujumbura baada ya kukutana na maafisa wa usalama katika jimbo la kaskazini la Kayanza.
Serikali ya Rwanda imesema imesikitishwa na hatua hiyo ya upande mmoja iliyochukuliwa na Burundi ya kufunga mpaka wa pamoja wa nchi mbili.
Taarifa iliyotolewa na serikali ya Kigali imesema, uamuzi huo utakwamisha harakati za kuingia na kutoka za watu pamoja na uingizaji na utoaji wa bidhaa katika nchi mbili na vilevile unakiuka misingi ya ushirikiano wa kikanda na utangamano wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, EAC.
Kundi la waasi la RED-Tabara, linalotuhumiwa kuhusika na shambulio baya la Desemba 22, 2023 nchini Burundi, lina makao yake mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, na limekuwa likipambana na serikali ya Burundi tangu mwaka 2015. Shambulizi la hivi majuzi lililofanywa na kundi hilo liliua watu 20, wakiwemo wanawake na watoto.
Kundi hilo lililojitokeza mwaka 2011 linakadiriwa kuwa na wapiganaji 500 hadi 800.
Rwanda inapakana na Burundi upande wa kaskazini. Mataifa hayo mawili yana mpaka wa pamoja wenye urefu wa kilomita 315.../