Baraza jipya la mawaziri latangazwa mashariki mwa Libya
Baraza jipya la mawaziri nchini Libya limeidhinishwa na Bunge lenye makao yake makuu mashariki mwa nchi hiyo, hatua ambayo inaweza kuzua wakati wowote mvutano mkubwa na serikali ya umoja wa kitaifa inayoongozwa na Waziri Mkuu Abdulhamid Dbeibah huko Tripoli.
Kwa mujibu wa spika wa bunge Aguila Saleh, wajumbe 92 wamepiga kura za 'ndiyo' kuidhinisha siku ya Jumanne baraza hilo jipya litakaloongozwa na aliyekuwa waziri wa mambo ya ndani Fathi Bashagha.
Kubuniwa kwa serikali ya Bashagha kunaashiria mawaziri wakuu wawili nchini humo suala ambalo wachambuzi wanasema huenda likazua upya ghasia nchini humo.
Mwanzoni mwa mwezi Februari, Bashagha alipewa jukumu la kuunda serikali mpya itakayochukua nafasi ya ile ya Dbeibah ambayo alitakiwa aondoke madarakani baada ya uchaguzi ulioahirishwa mwezi wa Desemba. Dbeibah amerudia mara kadhaa kusema kwamba ataacha madaraka baada ya uchaguzi mkuu na kukabidhi utawala kwa seriali itakayochaguliwa na raia.
Dbeibah ambaye pia ni tajiri mkubwa wa ujenzi alichaguliwa mwaka mmoja uliopita ikiwa sehemu ya juhudi za Umoja wa Mataifa za kurejesha utulivu nchini Libya kufuatia mapinduzi ya mwaka wa 2011, yaliyomuondoa madarakani kiongozi wa muda mrefu Kanali Muammar Gadafi.
Jukumu kubwa la Dbeibah lilikuwa ni kuongoza taifa hilo kwenye uchaguzi mwezi Desemba, lakini ukaahirishwa.../