Watu 18 waaga dunia baada ya mgodi wa dhahabu kuporomoka Guinea
(last modified Fri, 04 Mar 2022 02:38:36 GMT )
Mar 04, 2022 02:38 UTC
  • Watu 18 waaga dunia baada ya mgodi wa dhahabu kuporomoka Guinea

Wachimba migodi wasiopungua 18 wamefariki dunia baada ya kuporomokewa na udongo kwenye mgodi wa dhahabu magharibi mwa Guinea.

Hayo yalisemwa jana Alkhamisi na Ousmane Gaoual Diallo, msemaji wa serikali ya Guinea Conakry na kuongeza kuwa, ajali hiyo ilitokea Jumatatu katika eneo la Gaoual, yapata kilomita  386 kutoka Conakry. 

Amesema shughuli za kujaribu kutafuta miili zaidi katika mgodi huo zilikuwa zinaendelea hadi jana Alkhamisi, na wana wasiwasi kuwa yumkini idadi ya walioaga dunia kwenye mkasa huo ikaongezeka.

Guinea ni moja ya nchi za bara Afrika zenye utajiri mkubwa wa madini hususan dhahabu, ingawaje shughuli za uchimbaji madini katika aghalabu ya matimbo ya nchi hiyo ya Afrika zinafanyika kinyume cha sheria na bila ya uangalizi wa vyombo vya dola.

Migodi haramu ya dhahabu

Mwezi Mei mwaka jana, kwa akali watu 15 walipoteza maisha kwenye ajali nyingine ya kuporomoka kwa mgodi wa dhahabu katika eneo la Siguiri, kaskazini mashariki mwa Guinea.

Takwimu zinaonyesha, aghalabu ya madini hususan ya dhahabu yanayochimbwa kinyume cha sheria nchini humo pamoja na nchi nyingine za Afrika, husafirishwa kimagendo katika nchi za Ulaya na Uarabuni.