Maandamano ya kulaani ongezeko la visa vya uhalifu yafanyika Afrika Kusini
Mamia ya watu wamefanya maandamano nchini Afrika Kusini kulalamikia ongezeko la visa vya uhalifu wanavyodai kuwa vinafanywa na raia wa kigeni nchini humo.
Wakazi wa eneo la Diepsloot, viungani mwa jiji la Johannesburg, walifanya maandamano hayo jana Jumatano, huku wakilikosoa jeshi la polisi la nchi hiyo kwa kushindwa kukabiliana na wahajiri hao wanaotuhumiwa kufanya jinai na visa vya kihalifu.
Mmoja wa waandamanaji ameviambia vyombo vya habari kuwa, "tumechoka na wahamiaji haramu wanaoishi katika jamii zetu. Wao ndio wanaofanya aghalabu ya uhalifu kwa kuwa wanajua hawawezi kufuatiliwa kwa kutumia alama za vidole."
Waandamanaji hao wamedai kuwa, watu saba waliuawa mwishoni mwa wiki katika eneo la Diepsloot, viungani mwa jiji la Johannesburg, lakini hakuna mshukiwa yeyote aliyetiwa mbaroni na polisi mpaka sasa.
Askari polisi wa Afrika Kusini walilazimika kutumia risasi za plastiki na mabomu ya gesi ya kutoa machozi kuwatawanya waandamanaji hao waliokuwa na ghadhabu, ambao walikuwa wamefunga barabara na kuchoma moto matairi.
Wahajiri kutoka nchi za Afrika kwa muda mrefu sasa wamekuwa wakituhumiwa kufanya uhalifu nchini Afrika Kusini, mbali na kuchukua nafasi za ajira ambazo wenyeji wanadai walipaswa kupewa wao. Waafrika Kusini wamekuwa wakituhumiwa pia kuwafanyia ubaguzi na kuwashambulia wageni.