Utafiti: Mabadiliko ya tabianchi yameshadidisha vimbunga Afrika
Timu ya kimataifa ya wanasayansi wa hali ya hewa imesema vimbunga vilivyoshuhudiwa katika miezi ya hivi karibuni katika nchi za kusini mwa Afrika vilisababishwa na mabadiliko ya tabianchi.
Utafiti uliofanywa na taasisi ya kimataifa ya World Weather Attribution umeonyesha kuwa, vimbunga vya kitropiki vilivyohudiwa katika nchi za Madagascar, Malawi, na Msumbiji mapema mwaka huu vilisababishwa na ongezeko la joto katika sayari ya dunia.
Katika kipindi cha wiki sita baina ya Januari na Machi mwaka huu, eneo hilo la kusini mwa Afrika lilishuhudia vimbunga vitatu vya kitropiki na madhoruba mawili ya kitropiki.
Vimbunga hivyo vilisababisha mvua kubwa na mafuriko yaliyoua watu zaidi 230, mbali na kusababisha malaki ya wengine kupoteza makazi yao katika eneo hilo la kusini mwa Afrika.
Ripoti mpya ya jopo la kimataifa kuhusu mabadiliko ya tabianchi IPCC imeonya kuwa, mabadiliko ya tabianchi yanayochochewa na shughuli za binadamu yanasababisha usumbufu wa hatari na kuathiri maisha ya mabilioni ya watu kote ulimwenguni.
Mabadiliko ya tabianchi yamekuwa na athari tofauti katika maeneo mbalimbali ya dunia, kiasi kwamba katika baadhi ya maeneo yanasababisha ongezeko la joto, maeneo mengine yamesababisha mvua za masika na maeneo mengine yanasababisha ukame.