Apr 20, 2022 02:46 UTC
  • Kuendelea mivutano ya kisiasa nchini Libya

Mivutano ya kisiasa imeongezeka huko Libya ambapo serikali inayoongozwa na Fathi Pashaga, inailaumu Serikali ya Umoja wa Kitaifa kwa kuibua mivutano hiyo na kutahadharisha kuwa serikali hiyo itabeba dhima ya tukio lolote litakalohatarisha maisha ya Walibya.

Katika hali ambayo Fathi Pashaga alichaguliwa na wingi wa kura za wabunge wa Libya  mnamo Februari 10, 2022 kuwa waziri mkuu mpya alitakuwa kuchukua nafasi ya Abdul Hamid al-Dbeibah, Waziri Mkuu wa Serikali ya Muda, lakini Al-Dubaiba ilikataa kukabidhi madaraka kwa serikali hiyo mpya na kusisitiza kuwa atakabidhi tu madaraka hayo kwa serikali ambayo itachaguliwa na wananchi.

Mivutano hiyo inaendelea katika hali ambayo nchi hiyo ilikuwa inajiandaa kufanya uchaguzi ambao ungemaliza vita na hitilafu za ndani ambazo zimedumu kwa miaka mingi na kuvuruga usalama na uchumi wa nchi hiyo. Pamoja na hayo lakini uchaguzi huo uliotarajiwa kufanyika mwezi Disemba uliopita haukufanyika na hivi sasa nchi hiyo imetumbukia kwenye mivutano mipya ya kisiasa ambapo Fathi Pashaga anamtuhumu al-Dbeiba kuwa ameghusubu madaraka na kwamba hana uhalali wowote wa kisheria wa kuongoza Libya. Amesema kwa kuwa hataki kukabidhi madaraka kwa njia ya amani atabeba dhima ya ghasia zozote za kiusalama na kisiasa zitakazotokea nchini.

Mazungumzao ya kuzipatanisha pande hasimu za Libya

Hali ya mambo huko Libya ni tata kwa sasa na inatishia kuharibu matunda yote ya kisiasa yaliyopatikana chini kufikia sasa. Katika hali ambayo Fathi Pashaga anafanya juhudi za kuingia katika mji mkuu wa Libya Tripoli kwa ajili ya kuanza kazi yake kama Waziri Mkuu, duru za libya zinasema kuwa idadi kubwa ya magari ya kijeshi yaliyobeba silaha nzito yameonekana yakiingia mjini humo kutokea pande za Magharibi na Kusini.

Kwa mujibu wa baadhi ya ripoti, wanamgambo hao wanafungamana na Serikali ya Umoja wa Kitaifa inayoongozwa na Abdul Hamid ad-Dbeibah na walisikika wakipiga nara za 'siku muhimu inawadia' walipokuwa wakiingia Tripoli. Pamoja na hayo, lakini juhudi za upatanishi wa kimataifa zingali zinaendelea kwa madhumuni ya kukabidhiwa madaraka nchini kwa njia ya amani.

Katika uwanja huo, Umoja wa Mataifa unaunga mkono pendekezo lililotolewa na Stephanie Williams, Mwakilishi Maalumu wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa nchini Libya, la kuunda kamati ya pamoja ya Bunge na Baraza la Serikali. Kwa msingi wa pendekezo hilo, kamati hiyo itakuwa na jukumu la kuandaa sheria ya kuandaa uchaguzi nchini Libya.

Stephanie Williams, aliandika kwenye ukurasa wake binafsi wa Twitter kwamba: Raia wengi wa Libya wanajua kwamba utatuzi wa mwisho wa mgogoro unaoikumba nchi yao ni kufanyika uchaguzi kwa kufuata misingi imara ya katiba na katika mfumo ambao utadhamini mchakato wa uchaguzi.

Wasiwasi umeongezeka kuhusiana na hatari ya kugawanyika Libya katika makundi makuu hasimu. Licha ya juhudi na upatanishi wote ambao umefanyika kwa shabaha ya kuleta amani ya kudumu Libya, lakini kungali kuna wasi wasi kwamba iwapo upatanishi huo utafeli uchaguzi uliopangwa kufanyika kwa ajili ya kubuni serikali kuu yenye nguvu na ya kidemokrasia hautafanyika na hivyo kuitumbukiza tena nchi hiyo katika vita vya wenyewe kwa wenyewe.

Abdul Hamid ad-Dbeibah (kushoto) na Fathi Pashaga

Ali al-Swalabi, mjumbe wa Umoja wa Kimataifa wa Wanazuoni wa Kiislamu na mchambuzi wa masuala ya Libya anasema: "Mapatano ya kijamii na kisiasa ndilo sharti kuu la hatua yoyote ya kisiasa kwa ajili ya kufikia utulivu nchini Libya. Hitilafu si tu kwamba zinazuia uchaguzi bali zitaibua mapigano ya kijeshi ambayo yataendelea kwa muda mrefu.

Hii ni katika hali ambayo kuongezeka mivutano kati ya makundi ya kisiasa ya Libya kumeongeza tena uingiliaji wa kigeni katika nchi hiyo ya Kiafrika, na hivyo kuzidisha harakati za makundi ya kigaidi yanayotumiwa na nchi za kigeni kupora utajiri wa Walibya.

Kinyume na matakwa ya raia wa Libya, ghasia na mivutano ya kisiasa imeongezeka tena nchini na hivyo kuongeza wasi wasi wa kuzuka tena machafuko na vita vya ndani katika nchi hiyo ya kaskazini mwa Afrika. Katika hali hiyo, ni wazi kuwa njia pekee ya kutatua mgogogo wa hivi sasa wa Libya ni kuandaliwa mazingira yanayofaa kwa ajili ya kufanyika uchaguzi huru na wa kidemokrasia na utakaoyaridhisha makundi yote ya kisiasa ya nchi hiyo.

 

Tags