Uturuki kufungua kituo cha kijeshi nchini Somalia
Serikali ya Uturuki imefungua ubalozi mpya nchini Somalia na kuahidi kufungua kituo cha kutoa mafunzo ya kijeshi katika nchi hiyo ya Pembe ya Afrika karibuni hivi.
Hayo yamesemwa na Rais Recep Teyyip Erdogan wa Uturuki ambaye aliwasili nchini Somalia jana Ijumaa kwa ziara rasmi ya kikazi. Akizungumza baada ya kufungua ubalozi mpya wa Uturuki mjini Mogadishu katika wilaya ya Abdulaziz, Erdogan alisema yumkini karibuni hivi atarejea nchini Somalia kufungua kituo cha kutoa mafunzo ya kijeshi. Hii ni mara ya tatu kwa Rais wa Uturuki kuitembelea Mogadishu. Mara ya kwanza aliitembelea nchi hiyo ya Kiafrika inayokabiliwa na harakati za kigaidi kutoka kundi la kitakfiri la al-Shabaab, alipokuwa Waziri Mkuu mwaka 2011, wakati ambapo nchi hiyo ilikuwa imekabiliwa na janga la ukame na baa la njaa. Safari ya Erdogan mjini Mogadishu imekuja siku moja baada ya Philip Hammond, Waziri wa Mambo ya Nje wa Uingereza kuitembelea nchi hiyo ya Pembe ya Afrika na kufanya mazungumzo na Waziri Mkuu Omar Abdirashid Sharmarke na maafisa wengine wa ngazi za juu wa nchi hiyo.
Baada ya kuhatimisha safari yake nchini Uganda, Rais wa Uturuki, Jumatano usiku aliwasili mji mkuu wa Kenya, Nairobi kuendelea na awamu ya pili ya safari yake kabla ya kueleke Somalia.