Jul 21, 2022 12:42 UTC
  • Waliouawa katika mapigano ya kikabila Sudan wapindukia 100

Idadi ya watu waliouawa katika machafuko ya kikabila katika jimbo la Blue Nile kusini mashariki mwa Sudan imeongezeka na kufikia watu 105.

Hayo yamesemwa na Jamal Nasser, Waziri wa Afya wa Sudan ambaye ameongeza kuwa, mbali na watu 105 kuuawa, wengine 291 wamejeruhiwa kwenye makabiliano hayo baina watu wa makabila la Hausa na Berti jimboni Blue Nile.

Nasser amebainisha kuwa, hali ya utulivu imerejea kwa kiasi fulani kwenye jimbo hilo, hususan baada ya kutumwa vikosi vya usalama kwenda kukabiliana na mapigano hayo.

Hata hivyo amesema changamoto kubwa inayowakabili kwa sasa ni sehemu ya kuwahifadhi wakimbizi wa ndani walioathirika na mapigano hayo yaliyoanza Julai 11.

Kiongozi wa jamii ya Wahausa katika jimbo hilo, Mohamed Noureddine amesema yumkini idadi ya wahanga wa mapigano hayo ikaongezeka, kwa kuwa watu kadhaa wametoweka kutoka na vita hivyo.

Wakimbizi wa ndani nchini Sudan

Kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa, watu zaidi ya 17,000 wamelazimika kuyahama makazi yao kutokana na mapigano hayo, huku hali ya wasiwasi ikienea katika maeneo mengine ya nchi.

Wadadisi wa mambo wanasema mapinduzi ya kijeshi ya mwaka jana, yaliyoongozwa na Jenerali Abdel Fattah al-Burhan, yalizua ombwe la usalama ambalo limechochea kuibuka tena kwa ghasia za kikabila, katika nchi ambayo mapigano makali yanazuka mara kwa mara kuhusu ardhi, mifugo, upatikanaji wa maji na malisho.

 

Tags