Askari wanne wauawa DRC na watu wanaoshukiwa kuwa wanamgambo wa Mai-Mai
Vijana wanaoaminika kuwa wameungana na wanamgambo wa kundi la Mai-Mai wamewaua maafisa wa polisi wanne na kuwajeruhi wengine watatu, kwenye kituo cha ukaguzi cha Kangote, katika mji wa Butembo, mkoani Kivu Kaskazini, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.
Duru za vyombo vya usalama zimeripoti kuwa, mbali na kuua na kujeruhi askari hao polisi, wanamgambo hao wamechoma gari nne za polisi aina ya jeep katika shambulio hilo lililofanywa hapo jana.
Vyombo hivyo vya usalama vimeongeza kuwa matukio hayo ya hujuma na mashambulio yameanza kutokana na uvumi kuhusu uwezekano wa kuwepo waasi wa kundi la ADF katika maeneo kadhaa ya wilaya ya Bulengera katika sehemu ya mashariki ya mji wa Butembo.
Ripoti zinasema, hofu ilitanda miongoni mwa raia na wakazi wa wilaya za pembezoni mwa mji huo wa Kivu Kaskazini ambapo wengi walihama usiku kuelekea wilaya zinazodaiwa kuwa salama.
Kwa mujibu wa duru za habari, vijana wengine walilala nje usiku wa Alhamisi kuamkia Ijumaa, wakiwasha moto kujiandaa kwa tukio lolote.
Mauaji ya jana yamejiri, wakati usiku wa kuamkia Jumatano iliyopita watu wanane wakiwemo askari polisi wawili na raia mmoja waliuawa katika shambulio la kigaidi la wanamgambo wa ADF walipovamia Gereza la Kakwangura mjini Butembo katika mkoa huohuo wa Kivu Kaskazini kwa lengo la kuwatorosha wanachama wenzao 13, wakiwemo wanawake 12.
Genge la ADF lilifanya hujuma hiyo siku chache baada ya wanachama wake kuvamia vijiji viwili mashariki ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na kuua watu wasiopungua 20.../