Bunge jipya la Senegal lina idadi kubwa ya wabunge wateule wanawake
(last modified Mon, 12 Sep 2022 02:19:55 GMT )
Sep 12, 2022 02:19 UTC
  • Bunge jipya la Senegal lina idadi kubwa ya wabunge wateule wanawake

Senegal leo Jumatatu inafungua pazia jipya wakati idadi kubwa ya wabunge wateule katika bunge jipya la nchi hiyo watakapoanza shughuli zao, na hivyo kutoa matumaini ya kujiri mabadiliko katika nchi hiyo ambayo sheria na mitazamo ya mfumo dume imekita mizizi. 

Zaidi ya asilimia 44 ya viti vya uwakilishi katika Bunge Jipya la Taifa la Senegal vitawakilishwa na wabunge wanawake; idadi ambayo ni kubwa sana kuwahi kushuhudiwa katika nchi za Magharibi mwa Afrika. 

Bi Aminata Toure Waziri Mkuu wa zamani na mbunge mpya kutoka chama cha  APR cha Rais Macky Sall  ametahadharisha kuwa katika siasa wanasiasa wa kike siku zote hukabiliwa na changamoto ya upinzani na kutoaminiwa."  

Aminata Toure, Waziri Mkuu wa zamani wa Senegal 

Viti 73 kati ya jumla ya 165 vya bunge jipya la Senegal vitashikiliwa na wabunge wanawake kufuatia uchaguzi wa bunge wa mwezi Julai nchini humo. Uchaguzi huo unatajwa kama msingi wa demokrasia na uthabiti katika eneo la magharibi mwa Afrika lililogubikwa na mizozo na tawala za kijeshi. Kwa mujibu wa Taasisi ya miungano ya mabunge yenye makao yake mjini Gevena Uswisi, Senegal inashika nafasi ya 4 barani Afrika na ya 18 duniani kwa kwa usawa wa kijinsia bungeni ikizitangulia Uswisi, Ufaransa, Uingereza na Marekani.