Oct 14, 2022 07:45 UTC
  • Bunge la Djibouti laiweka FRUD katika orodha ya makundi ya kigaidi

Bunge la Djibouti limeliweka kundi la wabeba silaha la Front for the Restoration of Unity and Democracy (FRUD) katika orodha ya magenge ya kigaidi.

Haya yanajiri chini ya wiki moja baada ya askari saba wa jeshi la Djibouti kuuawa katika shambulio lililosadikika kufanywa na genge hilo la waasi wanaobeba silaha kaskazini mwa nchi.

Katika shambulio hilo lililofanyika Ijumaa iliyopita katika kambi ya kijeshi ya Garabtisan, kaskazini mwa nchi hiyo ya Pembe ya Afrika, mbali na wanajeshi saba kuuawa, wanne walijeuhiwa huku sita wakitoweka.

Katika taarifa ya jana Alkhamisi, Bunge la Djibouti limesema kwamba, kwa kauli moja limepasisha kuitambua FRUD kama kundi la kigaidi.

Taarifa iliyotolewa hapo awali na Rais Ismail Omar Guelleh wa Djibouti ilisisitiza kuwa, wanamgambo wa kundi linalobeba silaha la FRUD ndio walioshambulia askari wa serikali huko Garabtisan wiki iliyopita. 

Wanajeshi wa Djibouti

Mashambulio ya aina hii ni nadra sana kuripotiwa nchini Djibouti, ambapo shambulio la mwisho kudaiwa kufanywa na kundi hilo ilikuwa Januari mwaka jana 2021.

Kundi la FRUD ambalo akthari ya wapiganaji wake wanatoka katika jamii ya Afar ya kaskazini mwa nchi, lilianzisha uasi dhidi ya serikali mwaka 1991, wakidai kupigania maslahi ya jamii hiyo mkabala wa jamii nyingine yenye idadi kubwa ya watu ya Issas.

 

Tags