Mahakama Nigeria yamuondolea mashitaka kiongozi wa harakati ya Biafra
Mahakama ya Rufaa ya Nigeria imemfutia mashitaka yote Nnamdi Kanu, kiongozi wa Watu wa Asili wa Biafra (IPOB), wanaotaka kujitenga eneo la kusini mashariki mwa nchi hiyo ya Afrika Magharibi.
Katika uamuzi huo wa jana Alkhamisi, majaji wa Mahakama ya Rufaa wamesema Nnamdi Kanu alikamatwa kinyume cha sheria, na kwamba serikali ilikiuka sheria kwa kumkamata kwa nguvu nchini Kenya na kumrejesha nchini humo kwa ajili ya kesi iliyokuwa ikimkabili.
Mwezi Juni mwaka jana 2021, Nnamdi Kanu ambaye pia ana uraia wa Uingereza, alikamatwa nchini Kenya na kurejeshwa Nigeria. Alikimbilia Kenya baada ya korti kumuachia huru kwa dhamana.
Nnamdi Kanu anayengoza chama cha Indigenous People of Biafra (IPOB), alikuwa anakabiliwa na tuhuma za "ugaidi", uhaini na kueneza uongo dhidi ya Rais Muhammadu Buhari, hasa kupitia matangazo kwenye kituo cha Radio Biafra na mitandao ya kijamii.
Baada ya kukaa kizuizini kwa miaka miwili, Kanu alitoweka Aprili 2017 baada ya kuachiwa huru kwa dhamana. Wafuasi wake waliilaumu serikali ya Nigeria lakini yapata mwaka mmoja baadaye alijitokeza kwa njia ya kustaajabisha akiwa Israel. Januari 2017, Mahakama ya Juu ya Nigeria aliipiga marufuku harakati ya watu wa Biafra na kuliweka katika orodha ya makundi ya kigaidi.
Vita vya wenyewe kwa wenyewe vilivyodumu kwa miezi 30 ambavyo vilichochewa na matakwa ya kujitenga eneo la Biafra vilimalizika mwaka 1970. Inakadiriwa kuwa zaidi ya watu milioni moja waliaga dunia katika vita hivyo.
Eneo hilo ambalo ni makazi ya watu wa jamii ya Igbo, kabila la tatu kwa ukubwa nchini Nigeria, liliunganishwa tena na nchi hiyo lakini harakati za kutaka kujitenga zilianza tena baada ya mabadiliko ya utawala mwezi Mei 1999. Wanachama wa IPOB wanasema eneo hilo limetengwa kiuchumi na kisiasa tangu baada ya kumalizika vita vya wenyewe kwa wenyewe.