Idadi zaidi ya polisi watumwa mashariki mwa Kongo DR
Vyombo vya usalama vya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo vimetangaza kuwa askari zaidi wa jeshi la Polisi wametumwa eneo la mashariki mwa nchi hiyo.
Kwa mujibu wa duru za usalama, askari hao wametumwa eneo la Ntoto lililoko katika mkoa wa Kivu Kaskazini kwa lengo la kudhamini usalama wa wakaazi wa eneo hilo.
Apollinaire Mibeko, Naibu Mkuu wa asasi ya kiraia katika eneo la Walikale lililoko katika mkoa wa Kivu Kaskazini amekaribisha hatua hiyo ya kutumwa askari wa jeshi la Polisi katika eneo la Ntoto na kueleza kuwa hatua hiyo itasaidia kurejesha amani na kuwezesha wakimbizi kurejea makwao katika eneo hilo.
Askari zaidi wa polisi wametumwa huo Ntoto wiki moja baada ya askari wa jeshi kutumwa katika eneo hilo. Kwa zaidi ya miaka 20 sasa, eneo la Ntoto linadhibitiwa na makundi ya wanamgambo ya Maï-Maï Raïa Mutomboki na Kifuafua. Raia wa eneo hilo wamedhuriwa na kuathiriwa na mashambulio ya makundi hayo kiasi kwamba wakaazi wake wengi wameamua kuhama makaazi yao kutokana na kukosekana usalama.../