Mwinyi: Tofauti za kidini zisiwagawanye Watanzania
Rais mstaafu wa awamu ya pili wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Ali Hassan Mwinyi ameshutumu vikali kile alichokitaja kuwa udini na kuwataka Watanzania kutoruhusu tofauti zao za kidini na kimadhehebu kuwa chanzo cha mgawanyiko miongoni mwao.
Mwinyi alitoa kauli hiyo jana usiku jijini Dar es Salaam, wakati wa dhifa ya futari iliyoandaliwa na kituo kimoja cha televisheni nchini humo. Mwinyi amewataka Watanzania bila kujali itikadi na dini zao kulinda na kutunza amani iliyopo kwa kuendelea kudumisha upendo na ukarimu miongoni mwao. Amesema kufanya hivyo ni katika kutekeleza maagizo na mafundisho yaliyomo kwenye vitabu vitakatifu.
Rais mstaafu wa awamu ya pili wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ameongeza kuwa na hapa tunamnukuu: “Tuwe wavumilivu, linapokuja suala la dini kila mmoja amuache mwenzake aabudu anachokiamini, itikadi za dini zisituvuruge, ” mwisho wa kunukuu.