Machafuko ya kabla ya uchaguzi Afrika Kusini
Machafuko na ghasia zimeripotiwa kupamba moto katika kipindi hiki cha kabla ya uchaguzi wa mabaraza ya miji nchini Afrika Kusini.
Kituo kikuu cha machafuko hayo kimeripotiwa kuwa ni mji mkuu wa nchi hiyo, Pretoria. Sababu kuu ya machafuko katika mji huo imetajwa kuwa ni uamuzi wa chama tawala cha ANC wa kumteua Angela Thoko Didiza kuwa mkuu wa mji huo.
Katika kipindi chote cha siku kadhaa zilizopita mitaa na barabara za mji mkuu wa Afrika zimefungwa na magari mengi yamechomwa moto. Vilevile mfuasi mmoja wa chama tawala cha ANC ameuawa katika mkutano wa kampeni za uchaguzi.
Kwa kutilia maanani matukio ya miezi kadhaa ya hivi karibuni wachambuzi wa mambo wanatabiri kuwa, kuna uwezekano wa kushindwa chama tawala katika uchaguzi ujao wa mabaraza ya miji. Uchunguzi wa maoni uliofanyika unaonesha kuwa, chama kikuu cha upinzani cha Democratic Alliance kinaongoza katika miji kadhaa mikubwa nchini Afrika Kusini ukiwemo wa Pretoria.
Huko Johannesburg pia kunashuhudiwa mchuano mkali baina ya vyama hivyo viwili, na chama cha Democratic Alliance kinashika nafasi ya pili kikiwa nyuma ya ANC kwa kura chache sana. Hii ni pamoja na kuwa, tangu baada ya kusambaratika utawala wa ubaguzi wa rangi nchini Afrika Kusini, chama cha African National Congress kimekuwa kikishinda zaidi ya asilimia 60 katika chaguzi zote za kidemokrasia.
Inaonekana kuwa mgawanyiko uliopo ndani ya chama cha ANC, ufisadi wa kifedha wa Rais Jacob Zuma na changamoto za kiuchumi na kijamii zilizopo nchini Afrika Kusini vimeathiri vibaya nafasi ya chama hicho tawala.
Hivi karibuni pia Mahakama ya Katiba ya Afrika Kusini ilitoa hukumu ikimtaka rais huyo kurejesha Euro milioni 20 alizozichota kutoka Hazina kwa ajili ya ukarabati wa nyumba yake binafsi.
Iwapo chama cha ANC kitashindwa kupata thuluthi mbili ya kura za uchaguzi wa Bunge basi hapana shaka kwamba nafasi ya chama hicho itatetereka sana nchini Afrika Kusini. Hii ni kutokana na ukweli kwamba, rais wa nchi na mawaziri wa serikali huchaguliwa kutoka kwenye chama kilichopata kura nyingi zaidi. Kwa msingi huo inatazamiwa kuwa, kutafanyika mabadiliko makubwa ya uongozi ndani ya chama tawala kwa shabaha ya kulinda nafasi ya chama hicho katika chaguzi zijazo.
Weledi wa mambo wanasema iwapo chama cha ANC hakitafanikiwa kupata matokeo ya kuridhisha katika uchaguzi wa mabaraza ya miji, chama hicho kitazidisha mashinikizo ya kumtaka Zuma ajiuzulu uongozi wa chama. Hasa kwa kutilia maanani kwamba, vyama viwili vikuu vya upinzani Economic Freedom Fighters (EFF) na Democratic Alliance vinamtaka Zuma ang'atuke madarakani. Wapiznani hao wanasisitiza kudumisha mapambano yao hadi Zuma atakapotambuliwa kuwa ni mhalifu katika kesi ya ubadhirifu wa mali ya umma.