Mshukiwa mkuu wa mauaji ya kimbari Rwanda akamatwa Afrika Kusini
Fulgence Kayishema, mmoja kati ya watuhumiwa wakuu wa mauaji ya kimbari ya Rwanda ya mwaka 1994 ambaye amekuwa akisakwa kwa udi na uvumba kwa miongo kadhaa sasa hatimaye ametiwa mbaroni nchini Afrika Kusini.
Hayo yalisemwa jana Alkhamisi na timu ya wapelelezi wa Umoja wa Mataifa na kueleza kuwa, Kayishema ambaye anakabiliwa na makosa ya mauaji, uhalifu wa kivita na dhulma dhidi ya binadamu alikamatwa jana (juzi Jumatano) katika mji wa Paarl katika mkoa wa Cape Town, kusini magharibi mwa Afrika Kusini.
Duru za habari zinaarifu kuwa, Kayishema amekamatwa katika operesheni ya pamoja ya mamlaka za Afrika Kusini na timu ya Mahakama ya Kimataifa inayowafuatilia watoro wa jinai za kivita (IRMCT).
Mwendesha Mashtaka Mkuu wa chombo hicho cha sheria cha Umoja wa Mataifa, Serge Brammertz amesema mtoro huyo amekuwa mafichoni kwa zaidi ya miongo miwil, na kukamatwa kwake kunatoa hakikisho kwamba hatimaye atakabiliwa na hatua za kisheria kwa jinai anazotuhumiwa kufanya.

Fulgence Kayishema anatuhumiwa kuratibu na kutekeleza mauaji ya takriban wakimbizi 2,000 wa Kitutsi katika Kanisa la Katoliki la Nyange, wakati wa kujiri mauaji ya kimbari ya Rwanda mwaka 1994. Amekuwa mbioni tokea Julai mwaka 2001.
Mauaji ya kimbari ya Rwanda yalitokea kwa muda wa siku 100 kuanzia Aprili 6 mwaka 1994 baada ya Rais Juvenal Habyarimana na mwenzake wa Burundi Cyprien Ntaryamira, wote Wahutu, kupoteza maisha wakati ndege yao ilipotunguliwa katika mji mkuu wa Rwanda, Kigali.