Jun 25, 2016 06:31 UTC
  • 14 wauawa katika mapigano Sirte, Libya

Kwa akali watu 14 wameuawa katika mapigano makali kati ya jeshi la Libya na wanachama wa kundi la kigaidi na kitakfiri la Daesh katika mji wa Sirte.

Taarifa ya jeshi hilo imesema magaidi 10 wameuawa katika makabiliano hayo yaliyofanyika jana Ijumaa katika mji huo wa bandari. Aidha taarifa hiyo imeongeza kuwa askari wanne wa vikosi vinavyounga mkono jeshi la Libya wameuawa katika mapigano hayo. Mei 20, vikosi hivyo vinavyounga mkono Serikali ya Umoja wa Kitaifa ya Libya vilianzisha operesheni ya kuuteka mji wa bandari wa Sirte, ambao kwa sasa uko chini ya udhibiti wa matakfiri wa Daesh.

Serikali ilitangaza siku ya Jumanne kwamba imewapoteza askari wake 18 katika mapigano mengine kati ya vikosi vya serikali ya nchi hiyo ya kaskazini mwa Afrika na wapiganaji wa Daesh, yaliyojiri katika mji wa Sirte. Vyanzo vya hospitali vinasema kuwa watu wengine 70 walijeruhiwa katika mapigano hayo. Kwa mujibu wa ripoti hiyo makumi ya matakfiri wa Daesh pia waliangamia katika mapigano hayo ya kudhibiti mji huo wa kistratajia.

Tags