Libya yawahukumu watu 37 kwa kusababisha vifo vya wahamiaji 11
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i99786-libya_yawahukumu_watu_37_kwa_kusababisha_vifo_vya_wahamiaji_11
Mahakama nchini Libya imeidhinisha hukumu kali kwa watu 37 waliotuhumiwa kujihusisha na magendo ya binadamu. Watu hao wanatajwa kusababisha vifo vya wahajiri waliokuwa wakijaribu kuelekea Ulaya kupitia Bahari ya Mediterania. Haya yameelezwa na Ofisi ya Mwendesha Mashtaka wa Libya.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Jul 11, 2023 11:02 UTC
  • Libya yawahukumu watu 37 kwa kusababisha vifo vya wahamiaji 11

Mahakama nchini Libya imeidhinisha hukumu kali kwa watu 37 waliotuhumiwa kujihusisha na magendo ya binadamu. Watu hao wanatajwa kusababisha vifo vya wahajiri waliokuwa wakijaribu kuelekea Ulaya kupitia Bahari ya Mediterania. Haya yameelezwa na Ofisi ya Mwendesha Mashtaka wa Libya.

Mahakama ya Rufaa katika mji wa al Bayda, umbali wa kilomita 800 mashariki mwa mji mkuu wa Libya, Tripoli imewahukumu watu hao 37 wenye mfungamano na genge la uhalifu lililoratibu safari ya wahajiri 11 walioaga dunia baharini wakisafirishwa kwa boti iliyochakaa. 

Wahajiri wa Kiafrika wanaojaribu kuelekea Ulaya 

Ofisi ya Mwendesha Mashtaka wa Mahakama hiyo ya Rufaa ya Libya ambayo haikutaja uraia wa watuhumiwa hao, imesema kuwa watu 37 wamepatikana na hatia; 5 miongoni mwao wakiwa wamehukumiwa kifungo cha maisha jela, 9 kifungo cha miaka 15, na waliosalia kifungo cha mwaka mmoja jela. 

Libya inatumika kama nukta kuu ya kuanzia safari ya makumi ya maelfu ya wahajiri wanaojaribu kuelekea barani Ulaya. Wahajiri hao aghalabu yao hutoka katika nchi za Afrika chini ya jangwa la Sahara. 

Libya imekuwa kituo cha magendo ya binadamu na usafirishaji haramu wa wahajiri wa Kiafrika kuelekea Ulaya baada ya mgogoro wa nchi hiyo mwaka 2011 ulioibua hali ya mchafukoge nchini. 

Ripoti ya mwezi Machi mwaka huu ya Umoja wa Mataifa kuhusu haki za binadamu huko Libya imedai kuwa wahajiri waliotelekezwa Libya wamekuwa wakifanywa watumwa wa ngono ambao ni uhalifu dhidi ya binadamu.