Jun 16, 2024 06:25 UTC
  • Wanadiplomasia waandamizi wa Iran na Imarati wajadiliana maendeleo ya kikanda 

Wanadiplomasia wakuu wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na Umoja wa Falme za Kiarabu wamefanya mazungumzo kwa njia ya simu na kujadiliana matukio ya hivi karibu katika eneo hili na masuala yenye maslahi kwa pande zote mbili.

Kaimu Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Ali Bagheri Kani na Waziri wa Mambo ya Nje wa Imarati, Sheikh Abdullah bin Zayed Aal Nahyan wamejadiliana hali mbaya iliyosababishwa na vita vya mauaji ya halaiki ya utawala katili wa Israel katika Ukanda wa Ghaza wakati wa mazungumzo yao hayo simu.

"Ni lazima kwa nchi za Kiislamu kutumia haraka sana suhula zote zilizopo ili kukomesha mauaji ya halaiki yanayofanywa na Wazayuni huko Ukanda wa Ghaza na kuwasaidia watu wanaodhulumiwa wa eneo hilo," amesisitiza Kaimu Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran Ali Bagheri Kani.

Kwa upande wake, Waziri wa Mambo ya Nje wa Imarati amegusia mkutano wa kilele wa Jordan kuhusu Palestina, na kusisitizia haja ya kupeleka misaada ya kibinadamu na kuchukua hatua madhubuti za kukomesha mashambulizi wanayoyaendelea ya Wazayuni huko Ukanda wa Ghaza.

Amesisitiza kuwa, Umoja wa Falme za Kiarabu unafanya kila uwezalo kujaribu kusimamisha vita na kutuma misaada ya kibinadamu kwa watu madhulumu na wasio na ulinzi wa Ukanda wa Ghaza.

Utawala katili wa Israel unaendesha vita vyake vya kikatili dhidi ya watu wa Ghaza tangu tarehe 7 Oktoba, mwaka jana baada ya Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina (Hamas), kuendesha operesheni ya kimbunga cha al Aqsa ambayo haijawahi kushuhudiwa mfano wake ili kulipiza kisasi cha ukatili uliokithiri wa Israel dhidi ya watu wa Palestina.