Iran na Libya zatangaza azma ya kuimarisha uhusiano
Mawaziri wa Mashauri ya Kigeni wa Iran na Libya wamesisitiza azma ya viongozi wa nchi mbili ya kupanua uhusiano wa pande mbili.
Hayo yamesemwa leo Jumanne baada ya Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran Hossein Amir Abdollahian kumkaribisha mwenzake wa Libya, Najla Mangoush mjini Tehran, ambapo pande hizo mbili zimejadili masuala mbalimbali ya uhusiano wa pande mbili na matukio ya kieneo na kimataifa.
Akielezea kufurahishwa kwake na hali ya usalama na amani nchini Libya, Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Iran ametangaza utayarifu wa Jamhuri ya Kiislamu kwa ajili ya kupanua uhusiano na nchi rafiki ya Libya na kusaidia katika ujenzi mpya wa nchi hii.
Amir Abdollahian amebainisha nafasi ya juu ya mwanamke nchini Iran na kukosoa sera za kinafiki na kindumakuwili za nchi za Magharibi na jinsi zinavyotumia kisiasa suala la haki za wanawake.
Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Iran pia amelaani kitendo cha kuchomwa moto Qur'ani Tukufu katika nchi za Sweden na Denmark na kusema, kuna umuhimu sana wa kuwepo mshikamano na umoja wa nchi za Kiislamu duniani katika uwanja huu.
Kwa upande wake, Waziri wa Mambo ya Nje wa Libya, Bi Najla Mangoush ameelezea kufurahishwa kwake na safari yake mjini Tehran, baada ya takriban miaka 17 tangu ziara ya mwisho iliyofanywa na afisa wa ngazi za juu wa Libya nchini Iran na kusema: Safari hii inaonyesha nia ya nchi mbili kupanua zaidi uhusiano wao.
Mawaziri wa Mambo ya Nje wa Iran na Libya wameafikiana kuhusu suala la kustawisha ushirikiano kati ya nchi hizo mbili katika nyuga mbalimbali, ikiwa ni pamoja na kuanzisha Kamisheni Kuu ya Pamoja, kuunda kamati ya mashauriano ya kisiasa, kuimarishwa uhusiano wa kiuchumi na kibiashara, ushirikiano wa kisayansi na kiteknolojia, na kufanyika maonyesho maalumu.