Sep 08, 2023 07:33 UTC
  • Iran yalaani shambulio la kigaidi lililoua makumi ya watu Burkina Faso

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amelaani vikali shambulio la kigaidi lililouwa makumi ya watu nchini Burkina Faso.

Nasser Kan'ani, Msemaji wa Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa, shambulio hilo la kinyama nchini Burkina Faso kwa mara nyingine tena limeonyesha kuwa, ugaidi na uchupaji mipaka ni tishio kwa ulimwengu mzima.

Sanjari na kutoa mkono wa pole na kutangaza kuwa pamoja na serikali na wananchi wa Burkina Faso kufuatia hujuma hiyo, Kan'ani ameeleza kuwa, shambulio hilo limethibitisha kwamba, kuna haja ya kuweko vita na mapambano athirifu sambamba na ushirikiano wa jamii ya kimataifa dhidi ugaidi.

Kwa akali maafisa usalama 53 wa Burkina Faso wameuawa katika makabiliano makali baina yao na genge moja la wanamgambo kaskazini mwa nchi. Mtandao wa kigaidi wa al-Qaida umetangaza kuhusika na shambulio hilo la kikatili katika eneo la Koumbri, mkoa wa Yatenga.

Wanajeshi wa Burkina Faso kazini

Duru moja ya serikali ilisema kuwa, makumi ya magaidi waliangamizwa na vikosi vya ulinzi na usalama vilivyojibu mashambulizi hayo. Magaidi zaidi ya 50 waliuawa wa na wengine 30 wamejeruhiwa katika mapigano hayo yaliyotokea baina yao na jeshi la Burkina Faso Jumatatu wiki hii kwenye eneo la Koumbri la jimbo la Yatenga, kaskazini mwa nchi hiyo.

Aidha mwanzoni mwa mwezi Juni mwaka huu, takriban watu 40, wakiwemo wasaidizi wa jeshi, waliuawa katika mashambulizi mawili ya kigaidi yaliyotokea kaskazini magharibi mwa Burkina Faso.

Tangu mwaka 2015, nchi ya Burkina Faso ya magharibi mwa Afrika haina usalama. Mashambulizi ya kigaidi yanatokea mara kwa mara na yameshasabasisha vifo vya watu wengi na kupelekea maelfu ya wengine kuyahama makazi yao.

Tags