Iran kujiunga na mfumo wa BRICS PAY ili kukwepa vikwazo vya Marekani
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i102910-iran_kujiunga_na_mfumo_wa_brics_pay_ili_kukwepa_vikwazo_vya_marekani
Spika wa Bunge la Iran, Mohammad Bagher Qalibaf amesema Iran itajiunga na BRICS PAY, mfumo wa kibenki wa kielektroniki unaotumiwa na muungano wa BRICS wa mataifa yanayoinukia kiuchumi, ili kukwepa vizuizi vya kibenki vilivyosababishwa na vikwazo vya Marekani.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Oct 01, 2023 03:52 UTC
  • mad Bagher Qalibaf
    mad Bagher Qalibaf

Spika wa Bunge la Iran, Mohammad Bagher Qalibaf amesema Iran itajiunga na BRICS PAY, mfumo wa kibenki wa kielektroniki unaotumiwa na muungano wa BRICS wa mataifa yanayoinukia kiuchumi, ili kukwepa vizuizi vya kibenki vilivyosababishwa na vikwazo vya Marekani.

Akizungumza katika kikao cha wazi cha Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu, Bunge la Iran, Qalibaf amesema kuwa Iran itajiunga na BRICS PAY kuanzia Januari 1, 2024.

"Hiyo inatupa fursa kubwa ya kufanya kazi na nchi kubwa," amesema Qalibaf akifafanua juu ya kukua kwa biashara kati ya Iran na wanachama wa sasa wa BRICS, yaani Brazil, Russia, India, China na Afrika Kusini.

Mnamo Agosti 24 BRICS iliafiki wanachama wapya ambao ni Argentina, Misri, Ethiopia, Jamhuri ya Kiislamuu ya Iran, Saudi Arabia na Umoja wa Falme za Kiarabu ambazo zimealikwa kujiunga na kundi hilo.

Uanachama wa Iran ulikuja karibu miezi miwili baada ya kujiunga na Jumuiya ya Ushirikiano ya Shanghai, kambi inayoongozwa na nchi zenye uchumi mkubwa kama Uchina, Russia na India.

Qalibaf alisema hayo kuhusu BRICS PAY baada ya ziara yake nchini Afrika Kusini ambako alihudhuria mkutano wa maspika wa bunge la BRICS.

Alisema utumiaji wa Iran mfumo huo wa benki utaondoa haja ya kutumia SWIFT, mfumo wa ujumbe wa kifedha wa Ubelgiji ambao umeipiga marufuku Iran kutoka kwa huduma zake katika miaka iliyopita kwa sababu ya vikwazo vya Marekani.

Spika wa Bunge la Iran amesema China, Russia, India na Afrika Kusini zinachukua asilimia 30 ya biashara nzima ya Iran, na kuongeza kuwa BRICS PAY itakuwa chachu kubwa kwa juhudi za Iran za kudumisha na kuongeza uhusiano wake wa kibiashara na mataifa mengine duniani.

Alielezea kuundwa kwa mfumo wa malipo kama mafanikio makubwa kwa BRICS kwa sababu utarahisisha biashara kwa kupunguza haja ya kutumia mifumo inayotawaliwa na nchi za Magharibi kama vile SWIFT.

Taarifa iliyotolewa kwenye tovuti ya BRICS PAY inasema mfumo huo unalenga kuwezesha wafanyabiashara na watumiaji ndani ya jumuiya hiyo na zaidi ya hayo "kufanya na kupokea malipo kwa njia salama na bila ugumu katika sarafu zao za kitaifa" huku ukijaribu "kupunguza gharama na utata wa malipo ya kimataifa".