Jeshi la Iran lafanya 'Luteka ya Pamoja ya Droni 1402'
Vikosi vya Jeshi la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran vimeanza mazoezi makubwa ya pamoja ya kijeshi ya droni (ndege zisizo na rubani) katika eneo la kistratajia la Ghuba ya Uajemi na Bahari ya Oman.
Naibu Mkuu wa Uratibu wa Jeshi la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ametangaza habari ya kuanza mazoezi hayo ya pamoja na kueleza kuwa, luteka hiyo iliyoanza jana Jumanne inahusisha droni karibu 200.
Admeli Habibullah Sayyari amesema mifumo ya rada ya Meraj, Fatah-2, Bashir na Quds iliyotengenezwa na wataalamu wa humu nchini, sanjari na aina kadhaa za droni ni miongoni mwa suhula na zana za kivita zinazotumika kwenye maneva hayo.
Droni hizo, kwa mujibu wa Naibu Mkuu wa Uratibu wa Jeshi la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, ni pamoja na Chamorosh, Yasir, Sadeq, Pelican, Ababil-3, Yazdan, Ababil-4, Ababil-5, Kaman-12 (Bow-12), Kaman-19 na Mohajer-6.
Admeli Sayyari ameongeza kuwa, vikosi vinavyoshiriki kwenye luteka hiyo ya kijeshi ni pamoja na Kikosi cha Ulinzi wa Anga cha Jeshi la Iran, kitengo cha Anga za Mbali cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu la Iran (IRGC) na Kikosi cha Anga cha Jeshi la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.
Msemaji wa 'Luteka ya Pamoja ya Droni 1402' Brigedia Jenerali Alireza Sheikh amesema katika maneva hayo ya siku mbili, vikosi vya Iran vitaonyesha uwezo mkubwa wa mifumo ya kiulinzi na mifumo ya vita vya kielektroniki ya Jamhuri ya Kiislamu.
Amesema mazoezi haya ya kijeshi yanafanyika kwa kutegemea utaalamu wa wasomi wa ndani ya nchi katika kudhamini mahitaji ya kiulinzi, kwa shabaha ya kujiweka tayari kuzuia hujuma ya aina yoyote ya mabeberu wa kimataifa.