Nov 30, 2023 07:17 UTC
  • Iran: Hatima ileile ya kutoroka Afghanistan itawafika askari wa Marekani waliopiga kambi Iraq na Syria

Mshauri wa ngazi ya juu wa kijeshi wa Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullah Seyyed Ali Khamenei amepongeza Kambi ya Muqawama katika eneo na kusema "kutoroka" ndio hatima ya mwisho itakayovifika vikosi vamizi vya jeshi la Marekani nchini Syria na Iraq kama ilivyotokea Afghanistan.

Meja Jenerali Yahya Rahim Safavi amesema: “Muqawama wa wananchi na serikali za Iraq na Syria ndio uliopelekea kushindwa kwa DAESH (ISIS) ambao ni mamluki wa Kimarekani na Kizayuni; na Muqawama wa watu wa Afghanistan ndio uliosababisha kushindwa Marekani nchini humo na kupelekea watoroke kwa fedheha. Na ndio uliopelekea pia kufeli mipango ya Marekani ya kuipindua serikali ya Syria".

Rahim Safavi ameendelea kueleza kwamba, kilichosababisha kupunguzwa askari wa jeshi la Marekani nchini Iraq na Syria ni makundi ya muqawama katika nchi hizo na akaongeza kuwa, hatima ya mwisho ya wanajeshi wa Marekani ni kuikimbia Iraq na Syria kama walivyoikimbia Afghanistan.

Meja Jenerali Yahya Rahim Safavi

Kuna wanajeshi wapatao 2,500 wa Marekani nchini Iraq na wengine 900 nchini Syria kama sehemu ya kile Washington inachodai kuwa ni muungano wa kijeshi wa kupambana na DAESH. Marekani imeendeleza uwepo wake wa kijeshi katika nchi za Iraq na Syria, ingawa ukweli ni kwamba, ni nchi hizo mbili zenyewe za Kiarabu na washirika wao ndio waliowezesha kusambaratishwa kundi hilo la kigaidi mwishoni mwa 2017 baada ya kukalia maeneo ya ardhi za nchi hizo kwa miaka kadhaa.

Jenerali huyo wa ngazi za juu wa Iran amebainisha zaidi kwamba kushindwa utawala haramu wa Kizayuni wa Israel katika vita vya siku 33 na 55 katika Ukanda wa Gaza na kufeli kwake kufuatia Operesheni ya Kimbunga cha Al-Aqsa ni matokeo ya mapambano ya Kambi ya Muqawama.

Vile vile amesisitiza kuwa, mahubiri ya muqawama katika Ulimwengu wa Kiislamu ndio ufunguo wa umoja wa Waislamu kwa ajili ya ukombozi wa Quds tukufu.

Hisia za chuki dhidi ya Marekani zimeongezeka katika eneo la Asia Magharibi kwa wiki kadhaa sasa kufuatia uungaji mkono wa pande zote wa Washington kwa jinai za Israel katika Ukanda wa Gaza ambapo mashambulizi ya kinyama na ya mtawalia ya utawala huo wa Kizayuni yaliyoanza Oktoba 7, hadi sasa yameshasababisha Wapalestina zaidi ya 15,000 kuuawa shahidi.../

 

Tags