Dec 10, 2023 04:01 UTC
  • Raisi: Kimbunga cha al-Aqsa kimepanua mipaka ya muqawama

Rais wa Iran amesema Operesheni ya Kimbunga cha al-Aqsa imepanua mipaka ya muqawama na kuufikisha katika kona zote za dunia.

Rais Ebrahim Raisi amesema hayo hapa Tehran katika mazungumzo yake na  Hussein Arnous, Waziri Mkuu wa Syria na kuongeza kuwa: Hakuna shaka taifa la Palestina litaibuka mshindi katika vita vya Gaza, kama ambavyo mataifa ya eneo hili yatapata ushindi mkabala wa Marekani na waitifaki wake.

Raisi ameeleza bayana kuwa, utawala wa Kizayuni haujafikia chochote katika malengo yake, zaidi ya siku 60 baada ya kuanzisha hujuma za kinyama dhidi ya Gaza, isipokuwa kuua wanawake na watoto wasio na hatia. 

Sayyid Raisi amesisitiza kuwa, mauaji ya halaiki yanayotekelezwa na utawala haramu wa Israel dhidi ya wanawake na watoto wasio na hatia wa Kipalestina yatapelekea kuangamia utawala huo ghasibu.

Kadhalika Rais  wa Iran ameelezea kusikitishwa kwake na uungaji mkono unaotolewa na watu wanaojiita watetezi wa haki za binadamu, yaani Marekani na nchi za Magharibi, kwa mauaji ya kimbari ya Israel dhidi ya watu wa Palestina.

Mashahidi wa Gaza wamepindukia watu 17,700

Ameongeza kuwa, jinai za kutisha za utawala wa Kizayuni za kuwaua wanawake na watoto kwa himaya na uungaji mkono wa Marekani na nchi kadhaa za Ulaya, zimewashtua na kuwakasirisha watu wengi duniani dhidi ya utawala huo ghasibu.

Rais wa Iran amesisitiza kuwa, suala la Palestina daima linapaswa kuzingatiwa kuwa ni suala muhimu zaidi na kero kubwa ya nchi zote za Kiislamu.

Wakati huo huo, Rais wa Iran na Waziri Mkuu wa Syria wamezungumzia uhusiano wa pande mbili wa Tehran na Damascus na kusisitiza kuwa, ushirikiano wa mataifa haya mawili ya Waislamu umejengeka katika misingi imara na iliyokita mizizi.

 

Tags