Iran yaikosoa US kwa kuiweka Ansarullah katika orodha ya 'ugaidi'
(last modified Fri, 19 Jan 2024 03:30:33 GMT )
Jan 19, 2024 03:30 UTC
  • Iran yaikosoa US kwa kuiweka Ansarullah katika orodha ya 'ugaidi'

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amelaani vikali hatua ya Marekani ya kuiweka Harakati ya Ansarullah ya Yemen kwenye orodha ya kile inachokiita "makundi ya kigaidi" na kueleza kwamba, kitendo hicho ni katika mfululizo wa hatua za Washington za kuuunga mkono utawala wa kigaidi wa Israel.

Nasser Kan'ani, Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran ameeleza bayana kuwa, hatua hiyo ya Washington ya kuiweka Ansarullah katika orodha ya magaidi inaashiria namna Washington haina azma ya kurekebisha sera zake ghalati na haribifu katika eneo.

Shirika la habari la Mehr jana Alkhamisi lilimnukuu Kan'ani akisema kuwa, "Ansarullah na taifa la Yemen kwa ujumla linakabiliwa na hamaki za Marekani kwa sababu tu ya kuwanga mkono wananchi madhulumu wa Palestina."

Kan'ani ametilia shaka uhalali wa kimaadili wa serikali ya Marekani na kubainisha kuwa, watawala wa Washington hawana haki wala mamlaka ya kuwahukumu watu wengine. Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amesisitiza kuwa, hatua hiyo isiyo na maana ya Marekani ya kuiweka Ansarullah katika orodha ya 'ugaidi' haitateteresha msimamo wa wananchi wa Yemen wa kuwaunga mkono ndugu zao Wapalestina.

Wanajihadi wa Ansarullah wa Yemen

Jake Sullivan, mshauri wa usalama wa taifa wa Ikulu ya White House alitangaza usiku wa kuamkia jana Alkhamisi kwamba, Washington imeirejesha Harakati ya Ansarullah ya Yemen kwenye orodha ya kile kinachoitwa na nchi hiyo "makundi ya kigaidi".

Hii ni katika hali ambayo, Marekani iliiondoa Ansarullah katika orodha yake ya magaidi yapata miaka mitatu iliyopita. Rais wa Marekani Joe Biden alibatilisha uamuzi huo baada ya kuingia madarakani Januari 2021. 

Harakati ya Ansarullah ya Yemen imesema hatua hiyo ya Washington haina thamani wala itibari yoyote, na kwamba Yemen imekuwa chini ya mzingiro wa Marekani kwa miaka mingi. Ansarullah imesisitiza kuwa: kuchukuliwa hatua hiyo na Marekani kuhusiana na Ansarullah katika wakati huu kwa sababu ya msimamo wa harakati hiyo wa kuwaunga mkono watu wa Palestina ni sawa kutunukiwa nishani ya heshima na sharafu.  

Tags