Apr 09, 2024 08:05 UTC
  • Abdollahian: Marekani inapasa kuwajibishwa kwa shambulio dhidi ya ubalozi mdogo wa Iran

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran ameeleza kuwa serikali ya Marekani ina jukumu na inapasa kubeba dhima kwa shambulio la kigaidi katika ubalozi mdogo wa Iran mjini Damascus lililofanywa na utawala wa Israel unaotekeleza mauaji ya kimbari huko Gaza.

Hossein Amir Abdollahian ambaye jana alikuwa na mkutano na waandishi wa habari akiwa pamoja na mwenzake wa Syria, Faisal al Miqdad, huko Damascus amesema: Jinai ya kivita iliyofanywa na utawala ghasibu wa Israel kwa kutumia ndege na makombora yaliyoundwa Marekani dhidi ya sehemu ya ubalozi mdogo wa Iran mjini Damascus ni ukurasa mpya wa ukiukaji wa sheria za kimataifa na kinga za watu binafsi na maeneo ya kidiplomasia duniani; na utawala wa Kizayuni unaotekeleza mauaji ya kimbari Gaza utaadhibiwa.  

Amir Abdollahian ameongeza kuwa, hatua ya Marekani na nchi mbili za Ulaya ya kutokubali kutoa tamko la kulaani kukiukwa Mikataba ya Vienna na shambulio la utawala bandia wa Israel dhidi ya ubalozi mdogo wa Iran mjini Damascus ni ishara ya ridhaa na taa ya kijani ya Marekani kwa utawala dhalimu wa Kizayuni kwa ajili ya kutekeleza hujuma hiyo; na  Marekani ni lazima iwajibishwe kwa hatua yake hii na kuunga mkono jinai za utawala ghasibu wa Kizayuni. 

Katika mazungumzo hayo mjini Damascus, Faisal al Miqdad Waziri wa Mambo ya Nje wa Syria pia ameeleza kuwa utawala wa Israel unaotekeleza mauaji ya kimbari umejikita katika misingi ya chuki, nia mbaya na uchokozi; na umefanya kila jinai katika shambulio hilo huko Ukanda wa Gaza.

Faisal al Miqdad katika mazungumzo na Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran mjini Damascus

 

Tags