Apr 14, 2024 07:56 UTC
  • Kamanda wa IRGC: Iwapo Israeli itashambulia tena, itapokea jibu kubwa zaidi

Kamanda mwandamizi wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC) ameonya kwamba uvamizi wowote zaidi wa kijeshi utakaofanywa na utawala wa Israel utakabiliwa na jibu kubwa zaidi kutoka Iran.

Akizungumza na Press TV, kamanda mkuu wa IRGC amesema iwapo utawala wa Israel utafanya uchokozi wowote wa kijeshi katika ardhi ya Iran, basi Iran "itajibu kwa nguvu mara mbili."

Kauli yake hiyo imekuja baada ya IRGC kufyatua msururu wa makombora na ndege zisizo na rubani katika ardhi zinazokaliwa kwa mabavu kujibu hujuma ya kigaidi ya utawala wa Israel dhidi ya ubalozi mdogo wa Iran nchini Syria.

Mashambulio ya kulipiza kisasi ya Iran dhidi ya Israel yaliyopewa 'jina Operesheni ya Ahadi ya Kweli'  yametoa pigo kubwa kwa utawala huo wa Kizayuni.

Katika taarifa ya pili kufuatia operesheni hiyo, Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC) limesema: Operesheni hii imekuja baada ya siku 10 za "kimya na upuuzaji" wa mashirika ya kimataifa hususan Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa ambayo hayakulaani uvamizi wa Israel au kuuadhibu utawala huo kwa mujibu wa Kifungu cha 7 cha Mkataba wa Umoja wa Mataifa.

IRGC imesema Iran imefanya mashambulizi ya kulipiza kisasi, "ikitumia uwezo wake wa kimkakati wa upelelezi, makombora na ndege zisizo na rubani" kushambulia "ngome za jeshi la kigaidi la Kizayuni katika ardhi zinazokaliwa kwa mabavu. Nogme hizo zimepigwa kwa mafanikio na zimeangamizwa."

Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullah Seyyed Ali Khamenei, katika khutba yake ya Idul al-Fitr jijini Tehran Jumatano, alilitaja shambulio la Israel dhidi ya ubalozi mdogo wa Iran kuwa ni "kosa", ambalo aliahidi litakabiliwa na adhabu.

Wakati huo huo, Waziri wa Ulinzi wa Iran Brigedia Jenerali Mohammad Reza Ashtiani ameonya kwamba nchi yoyote itakayofungua ardhi au anga yake kwa utawala wa Israel kwa ajili ya mashambulizi [yanayoweza kutokea] dhidi ya Iran, itapata "jibu madhubuti."