Apr 15, 2024 08:09 UTC
  • Amir Abdollahian: Iran haikuwa na budi ila kuuadhibu utawala wa Kizayuni ndani ya fremu ya kujilinda halali

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amesema kuwa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran haikuwa na budi ila kuutia adabu utawala wa Kizayuni katika fremu ya kujilinda halali kufuatia Umoja wa Mataifa kunyamaza kimya na kushindwa kuchukua hatua za kidplomasia huku Baraza la Usalama la umoja huo likishindwa hata kutoa tamko la kulaani shambulio la utawala wa Israel katika ubalozi mdogo wa Iran huko Syria.

Shirika la habari la IRNA limeripoti kuwa, Hossein Amir Abdollahian amezungumza kwa njia ya simu na Josep Borrell Mkuu wa Sera za Nje wa Umoja wa Ulaya na kuashiria mashambulizi ya mara kwa mara ya utawala wa Kizayuni likiwemo shambulizi la utawala huo dhidi ya washauri wa kijeshi wa Iran wanaoshughulika katika vita dhidi ya ugaidi huko Syria na kusisitiza kuwa hujuma ya kijeshi ya utawala wa Kizayuni dhidi ya maeneo ya kidiplomasia ya Iran huko Damascus ni ukiukaji wa Mkataba wa Vienna na kuvuka mstari mwekundu wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. 

Amir Abdollahian amesisitiza kufanikiwa jibu la kijeshi la Iran katika fremu ya kujihami kihalali na kuongeza kuwa, baada ya kumalizika oparesheni hiyo; kumetolewa ujumbe huu kwamba kadhia hii imekwisha kwa mtazamo wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, lakini kama utawala wa Kizayuni utajibu mapigo, jibu la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran litakuwa la haraka, kubwa na la juu zaidi. 

Amir Abdollahian ameashiria hatua ya Umoja wa Ulaya ya kutoa taarifa ya kulaani shambulio la utawala wa Israel katika jengo la ubalozi mdogo wa Iran huko Damascus Syria na kueleza kuwa anataraji kuwa Umoja wa Ulaya unapaswa kuwasilisha mpango madhubuti na wenye athari ili kuhitimisha mauaji ya kimbari huko Ukanda wa Gaza ambapo Jamhuri ya Kiislamu ya Iran iko tayari kutoa mchango ili kufanikishwa mpango huo. 

Mauaji ya kimbari Ukanda wa Gaza 

Katika mazungumzo hayo ya simu, Josep Borrell Mkuu wa Sera za Nje wa Umoja wa Ulaya amesema kuwa umoja huo unaendeleza juhudi za kidiplomasia ili kuupatia ufumbuzi hali ya mgogoro katika Ukanda wa Gaza na kuhitimisha mateso yanayowakabili wakazi wa eneo hilo nametoa wito kwa Iran isaidie katika uwanja huo.