Apr 15, 2024 13:45 UTC
  • PressTV: Makombora yote ya hypersonic yaliyotumiwa na Iran dhidi ya Israel yalilenga shabaha + Video

Makombora yote ya hypersonic yaliyotumiwa katika mashambulizi ya Iran ya kuiadhibu Israel yamepiga malengo yaliyokusudiwa baada ya kukwepa mifumo ya ulinzi ya anga ya utawala huo harami na washirika wake.

Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran (IRGC) usiku wa kuamkia Jumapili ya jana lilifanya mashambulizi makubwa ya makombora na ndege zisizo na rubani katika maeneo yanayokaliwa kwa mabavu na Israel, ikiwa ni mara ya kwanza kwa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kutumia silaha hizo dhidi ya malengo halisi.

Operesheni ya mashambulizi hayo ya kulipiza kisasi, yaliyopewa jina la Operesheni True Promise, (Ahadi ya Kweli) ilisababisha uharibifu mkubwa katika kambi za kijeshi za Israel katika maeneo yote yanayokaliwa kwa mabavu.

Duru za habari zimearifu Press TV kwamba utawala wa Israel na waungaji mkono wake walishindwa kuzuia kombora lolote la hypersonic lililorushwa na Iran.

Iran ni miongoni mwa nchi chache ambazo zina teknolojia ya kutengeneza makombora ya hypersonic ambayo yanaweza kusafiri kwa kasi ya ajabu na kupiga shabaha kwa usahihi mkubwa.

Kwa mujibu wa shirika la habari la IRNA, kombora hilo lina kasi kubwa na uwezo wa aina yake, na hakuna teknolojia yoyote duniani inayoweza kulitungua hata katika kipindi cha miongo kadhaa ijayo.

Mkuu wa Majeshi ya Iran, Meja Jenerali Mohammad Baqeri, alisema Jumapili ya jana kwamba Iran imepiga kambi kubwa ya kijasusi ya Israel na kituo cha anga cha Nevatim Airbase, ambako ndege ya F-35 ilitokea na kulenga majengo ya kidiplomasia ya Iran huko Damascus.

Iran ilifanya mashambulizi hayo makini kulipiza kisasi cha hujuma hiyo ya kigaidi iliyoua shahidi washauri kadhaa wa kijeshi za Iran nchini Syria.