Apr 18, 2024 12:19 UTC
  • Kukiri Pentagon kuhusu uwezo wa kijeshi wa Iran katika kuujibu utawala wa Kizayuni

Patrick Ryder Msemaji wa Wizara ya Ulinzi ya Marekani (Pentagon) amekiri juu ya nguvu za kijeshi za Iran katika kutoa jibu la kijeshi kwa utawala wa Israel.

Msemaji wa Pentagon amekiri kuwa Iran ilifanya mashambulizi ya aina yake na makubwa kutokea ndani ya ardhi yake. Ryder ameeleza haya akibainisha ukubwa wa oparesheni ya kijeshi iliyotekelezwa na Iran kulipiza kisasi shambulio la Israel katika ubalozi wake mdogo huko Damascus, Syria.   

Patrick Ryder, Msemaji wa Pentagon 

Katika sehemu nyingine ya matamshi yake, Msemaji wa Wizara ya Ulinzi ya Marekani ameashiria mashauriano makubwa kati ya Waziri wa Ulinzi wa Marekani na wenzake kadhaa kuhusu eneo la Asia Magharibi na kudai kuwa Marekani inataka kupunguza mivutano ya kikanda na kuzuia pakubwa mapigano.  

Siku ya Jumamosi jioni na mapema Jumapili asubuhi, Kikosi cha Jeshi la Anga la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu la Iran (IRGC) lilitekeleza operesheni ya "Ahadi ya Kweli" ya kuuadhibu utawala wa Kizayuni na kufanikiwa kulenga shabaha ndani ya ardhi zinazokaliwa kwa mabavu na kuvurumisha makumi ya makombora na ndege zisizo na rubani (droni). Iran ilitangaza kuwa imetekeleza oparesheni hiyo ili kulipiza kisasi shambulio la makombora la Tel Aviv kwenye ubalozi mdogo wa Iran nchini Syria lililopelekea kuuliwa shahidi washauri 7 na maafisa wa kijeshi wa Tehran huko Damascus. Mwakilishi wa Kudumu wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika Umoja wa Mataifa pia ametangaza kuwa hatua ya kijeshi ya Iran ilitekelezwa kwa mujibu wa kipengee cha 51 cha Hati ya Umoja wa Mataifa kuhusu haki halali ya kujitetea katika kujibu uvamizi wa utawala wa Kizayuni dhidi ya maeneo ya kidiplomasia ya nchi hii. 

Nukta muhimu katika muktadha wa operesheni hii tajwa ya "Ahadi ya Kweli" ya kuiadhibu Israel ni misaada na uungaji mkono mkubwa wa Marekani, Uingereza na Ufaransa na baadhi ya nchi za eneo hili kwa utawala wa Kizayuni ili kukabiliana na ndege zisizo na rubani na makombora ya cruise na balistiki ya Iran.  Chanzo kimoja cha Habari nchini Marekani kimekiri kwamba nchi 10 ziliisaidia Israel kuzuia ndege zisizo na rubani na makombora ya Iran. Ni wazi kuwa  katika operesheni hii dhidi ya utawala wa Kizayuni, Iran ilikabiliana na NATO na Israel na waitifaki wao wa kieneo. Marekani ambayo ni mwanachama muhimu zaidi wa Muungano wa Kijeshi wa Nchi za Magharibi (NATO) ilitumia zana zake zote za ulinzi wa anga na za kuzuia makombora ili tu isaidie kuzuia na kuharibu ndege zisizo na rubani na makombora yaliyorushwa na Iran dhidi ya maeneo ya utawala wa Kizayuni. 

Droni na makombora ya kruzi na balistiki ya Iran dhidi ya Israel 

Pamoja na misaada na ungaji mkono mkubwa wa Marekani na nchi waitifaki wa Magharibi na baadhi ya nchi za eneo hili kwa utawala wa Kizayuni ili kuzuia droni na makombora ya kruzi na balistiki ya Iran pamoja na utawala huo kutumia kikamilifu suhula na zana zake zote za ulinzi wa anga na dhidi ya makombora lakini kivitendo makombora mengi yaliyovurumishwa na Iran yalifika na kulenga maeneo yaliyokusudiwa katika Palestina inayokaliwa kwa mabavu. 

Kuhusu kushindwa rada ya kisasa zaidi duniani kukabiliana na makombora ya Iran, Scott Ritter, mchambuzi mashuhuri wa masuala ya kijeshi wa Marekani anasema Marekani imeweka rada yake ya kisasa zaidi ya AN/TPY-2  katika jangwa la Negev na kwamba mfumo bora wa ulinzi wa makombora duniani ulishindwa kulinda maeneo ambayo yalikuwa na kazi ya kuzuia mashambulizi ya makombora ya Iran.   

Hii ni katika hali ambayo, licha ya madai kwamba utawala wa Kizayuni na waitifaki wake walisambaratisha asilimia 99 ya ndege zisizo na rubani na makombora ya kruzi na balistiki yaliyorushwa na Iran dhidi ya utawala wa Kizayuni lakini ukweli wa mambo ni tofauti kabisa. Kanali ya televisheni ya Marekani ya ABC ilitangaza katika ripoti yake kuwa, kufuatia operesheni ya pamoja ya ndege zisizo na rubani na makombora ya Tehran dhidi ya Tel Aviv, takriban makombora 9 yalipiga kambi mbili za anga za Israel na kusababisha uharibifu mkubwa kwa Tel Aviv. Televisheni hiyo iliarifu kuwa siku moja baada ya Iran kuupiga utawala wa Kizayuni kwa ndege zisizo na rubani na makombora; afisa mmoja wa ngazi ya juu wa Marekani alikiri kuwa kwa uchache makombora 4 ya balistiki ya Iran yalipiga kambi ya anga ya Israel ya Negev. Aliongeza kuwa makombora ya Iran yalipiga  njia ya uwanja wa ndege na ghala la kambi ya kijeshi ya Negev  na kusababisha uharibifu mkubwa. Ripoti hiyo pia imewanukuu maafisa wa kuaminika wa Marekani na kueleza kuwa makombora matano mengne pia yaliipiga kambi ya Nevatim ya kikosi cha anga cha utawala wa Kizayuni na kuharibu ndege ya usafiri ya C-130. 

Uwezo wa makombora wa Iran 

Kukiri Msemaji wa Pentagon kuhusu uwezo wa kijeshi wa Iran katika kukabiliana na utawala wa Kizayuni na kutekeleza mashambulizi makubwa na ambayo hayajawahi kushuhudiwa kutoka ndani ya ardhi ya Iran hadi Palestina inayokaliwa kwa mabavu licha ya kuarifiwa waitifaki wa kieneo wa Marekani kuhusu shambulio hilo masaa 72 kabla ya oparesheni hiyo ambayo bila shaka Marekani pia ilikuwa na taarifa kunaonyesha kuwa Iran ina uwezo wa kutoa vipigo vikali kwa adui licha ya maandalizi yote ya kijeshi ya Israel, Marekani na waitifaki wao wa kieneo na vilevile nchi za Ulaya.  

Scott Ritter, mchambuzi wa masuala ya kijeshi anaamini kuwa, kilichofanywa na Iran katika mashambulizi ya Jumamosi na Jumapili iliyopita dhidi ya maeneo ya utawala wa Kizayuni katika ardhi zinazokaliwa kwa mabavu ni kuhuisha nguvu za nchi hii za kukabiliana na hujuma dhidi yake. Ritter ameitathmini oparesheni ya "Ahadi ya Kweli" ya kutoa kipigo na kuiadhibu Israel kuwa iliyofanikiwa pakubwa, na kwamba tunaweza kusema kuwa oparasheni hii si tu imekuwa na mafanikio makubwa kwa Iran, bali kwa ulimwengu mzima kwa sababu uwezo wa sasa wa Iran wa kukabiliana na hujuma dhidi yake ni ukweli usio na shaka; uwezo ambao unaweza kuzidhibiti Marekani na Israel."

Tags